Wakati Serikali ikianza kutekeleza mpango wake
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao unalenga kukuza uchumi na kuboresha
maisha ya wananchi wake, imebainika kuwa Tanzania ina upungufu wa
waandisi 76,000.
Akizungumza hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa fani
hiyo nchini, Profesa Burton Mwamila ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wa
kwanza kuhitimu uhandisi hapa nchini, anasema mwaka 1973 walidahiliwa
wanafunzi 60, lakini hivi sasa chuo hicho kinapokea wanafunzi 600 ambao
ni idadi ndogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo hivi sasa.
“Taifa linapokuwa na wanafunzi wa uhandisi 600 wanaohitimu masomo kwa mwaka kati ya watu milioni 45 ni kidogo sana,” anasema.
Anasema ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo
iliyopo hivi sasa, Tanzania inahitaji waandisi 88,000, lakini waliopo ni
12,000 pekee.
Mwamila ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia, anasema kwamba wahandisi
wanapokuwa wachache hawawezi kufanyakazi kwa umakini kwa sababu
wanalazimika kufanya kazi nyingi, jambo linalowapunguzia ufanisi katika
kusimamia miradi wanayopewa.
“Kuna wakati mtalazimika kumtumia technian badala
ya mhandisi, tena wakati mwingine mtamtumia mhandisi kama technician
kwasababu hata wao hawatoshi,” anasema.
Kuhusu mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa;
Mwamila anasema ni muhimu kuwa na mipango ya maendeleo, lakini
anachokiona ni kuwa nchi za nje ndizo zitakazotoa mchango mkubwa katika
kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake.
Ili nchi ifanikiwe kuendesha miradi mikubwa ya
maendeleo bila kutegemea misaada kutoka nje ya nchi, unahitajika mpango
maalumu utakaowezesha udahili wanafunzi wengi wa uhandisi.
Hata hivyo, anasema kwamba njia sahihi ya
kufanikiwa kwenye mpango wa BRN ni kuwa na Watanzania watakaoweza
kuuendeleza mpango huo katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Walipotoka
Wanafunzi wa kwanza wa uhandisi Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, walidahiliwa mwaka 1973 wakiwa 60 ambapo hadi sasa wamebaki
48 baada ya 12 kufariki dunia.
Wataalamu hao ambao wengi wao wanasifika kwa
kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo hapa nchini, wanasema kitivo cha
uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzishwa kwa msaada wa
Serikali ya Ujerumani na kwamba hata walimu wake wengi walikuwa ni
kutoka nchini Ujerumani
Chanzo Na Goodluck Eliona, Mwananchi gazeti
Novemba16
2013
saa
11:33 AM
0 comments:
Post a Comment