....KITUO KUANZA KUJENGWA MWEZI UJAO!
....WAFANYAO VYEMA KWENDA SUNDERLAND ACADEMY OF LIGHT!!
HABARI
za uteuzi wa Kocha wa zamani wa Azam FC, Stewart Hall, kuwa Meneja wa
Kituo kipya cha Kidongo Chekundu Sports Park pamoja na Elite Football
Academy, zote za Mjini Dar es Salaam, zimeleta matumaini makubwa kwa
Soka la Tanzania.
Kituo cha Kidongo Chekundu Sports Park
kitaendeshwa kwa pamoja na Symbion Power, Wazalishaji wakubwa wa Umeme
Nchini, Klabu ya Sunderland ya England na Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo.
Matumaini haya makubwa yalitangazwa Juzi
na Mtendaji Mkuu wa Symbion Power Tanzania, Peter Gathercole, ambae
alisema kuwa Mradi huo utatoa fursa kwa Vijana ambao watafundishwa mbinu
za kiufundi, kiakili na kuwajenga kimwili ili wafanikiwe katika Soka la
sasa.
Gathercole pia alitoboa kuwa wale Vijana
watakaofanya vyema kwenye Kituo hicho watapelekwa kwenye Chuo cha Soka
cha Klabu ya Sunderland huko England kiitwacho Sunderland Academy of
Light.
Kituo cha Kidongo Chekundu Sports Park,
ambacho Umma utaruhusiwa kukitumia, kitakuwa na Uwanja mkubwa wa Soka
wenye Majani ya Bandia pamoja na Taa za kuchezea Usiku na pia vitakuwepo
Viwanja vidogo vitano ili kukidhi Marika ya Vijana wa Umri mbalimbali.
Pia, Kituo hicho kitakuwa na Vyumba vya Kubadili Jezi, Zahanati yenye zana zote na Mgahawa.
Ujenzi wa Kituo hiki utaanza Mwezi ujao.
Mkuu huyo wa Symbion Power, Peter
Gathercole, amesema uteuzi wa Stewart Hall ni hatua muhimu katika azma
yao wao, Sunderland na Serikali katika kuleta maendeleo kwa Vijana.
Stewart Hall, ambae ana Leseni ya Ukocha
ya UEFA ngazi ya Pro pamoja na Ukufunzi, aliondoka kuwa Kocha wa Azam
FC Wiki iliyopita na kabla ya hapo aliwahi kuwa Kocha wa Timu ya Taifa
ya Zanzibar.
Huko nyuma, Hall aliwahi kuwa Mkufunzi
kwenye Chuo cha Soka cha Klabu ya England, Birmingham City, Kocha wa
Timu ya Taifa ya Visiwa vya Saint Vincent and the Grenadines pamoja na
Klabu ya India, Pune FC.
Wakikaribisha hatua hii ya uteuzi wa
Hall, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Sunderland, Margaret Byrne, alituma
salaam za furaha na kuunga mkono kitu ambacho pia kilifanywa na Waziri
Fenella Mukangara wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mwezi Juni, Rais wa Tanzania Jakaya
Kikwete, pamoja na Waziri Fenella Mukangara walitembelea Sunderland
Academy of Light ambako waliunga mkono juhudi za Klabu hiyo na Symbion
Power katika kuendeleza Vijana kupitia Soka.
0 comments:
Post a Comment