>>ZIPO KESI 3 ZA OKWI FIFA!!
>>VPL: MECHI ZA TANZANIA PRISONS YAZASOGEZWA
SOMA ZAIDI:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Januari 22, 2014
USAJILI WA OKWI YANGA WAZUIWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji
Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri
ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya TFF iliyokutana leo (Januari 22 mwaka huu) kupitia masuala
mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi
aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.
Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu
yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa
kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda
kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel
likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
Katika FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na
suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa
kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro.
Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya
mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.
Hivyo, TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua
iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile
du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai
Okwi bado ni mchezaji wake.
MECHI ZA TANZANIA PRISONS YAZASOGEZWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limesogeza mbele mechi za raundi ya 14 na 15 zinazoihusu timu ya
Tanzania Prisons zilizokuwa zichezwe Januari 25 na 29 mwaka huu.
Awali Tanzania Prisons ilitakiwa
kutafuta uwanja mwingine wa kuchezea mechi hizo dhidi ya Ruvu Shooting
na JKT Ruvu kutokana na Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine kutokuwa tayari
kwa Ligi Kuu ya Vodacom wikiendi hii.
Mechi hizo sasa zitachezwa kati ya Februari 6 na 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Sokoine.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment