Thursday, 14 April 2016

Muda Wa Uzimaji Simu FEKI Hautaongezwa- Makame Mbarawa

  ;

Waziri  wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiiano Profesa Makame  Mbarawa amesema Serikali haitaongeza muda katika zoezi zima la uzimaji wa simu feki ifikapo Juni 16 mwaka huu.

Ameyasema hayo ofisini kwake leo jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha habari hapa nchini.

Amesema Serikali imeamua kuchukua uamuzi huo kutokana na madhara mbalimbali yatokanayo na simu hizo ikiwemo ya kiafya na kusisitiza kuwa serikali inapoteza mapato mengi kutokana na uingizwaji wa simu hizo nchini.

"Tunategemea kuzima simu zote feki kutokana na madhara yake kiafya  hasa kwa watumiaji, kukosekana kwa viwango vya ubora wa simu hizi na hivyo wananchi kupoteza fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa simu hizi kwani hufa mara kwa mara", amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ameongeza kuwa kwa sasa Jopo la wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) limepelekwa mkoani Singida kwa ajili ya kutoa elimu ya utambuzi wa simu hizo ili kuweza kuwasaidia wananchi kubaini kwa urahisi.

Amesisitiza wananchi kuchukua tahadhari kabla ya kununua simu ikiwemo kumuuliza muuzaji kabla ya kununua, kudai risiti na kuituinza ili kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa bidhaa hizo nchini.

Katika hatua nyengine, Waziri Mbarawa amesema kuwa suala la mkongo wa Taifa linaendelea vizuri ambapo Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano wanaendelea na usimikaji wa minara ya mawasiliano katika sehemu mbalimbali za nchi hususan vijijini ili kuleta huduma bora za mawasiliano nchini.

"Kwa sasa awamu ya nne ya mradi huu wa Mkongo wa Taifa unaendelea, kwani makampuni mbalimbali ya simu yanasimika minara yao katika sehemu mbalimbali za nchi ili kusambaza na kuboresha mawasiliano kwa wananchi", amefafanua Profesa Mbarawa.

Ameongeza kuwa  uwepo wa  mkongo huo nchini kumepelekea mapinduzi katika sekta ya mawasiliano, mabenki na kuiongezea Serikali pato kwani hata nchi za jirani hutumia mkongo huo katika kupata mawasiliano yaliyo bora.

Tathmini imebainisha kuwa kutokana na uwepo wa mkongo huo nchini watumiaji wa simu wamefikia milioni 39.7 na wa intaneti kufukia milioni 17.

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi)
 ;

0 comments: