;
SERIKALI imeanza kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii na hadi kufikia Machi, mwaka huu tayari imeshalipa Sh bilioni 173.11 kwa mfuko wa PSPF huku ikidhamiria kulipa deni lote kufikia Juni, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) mfuko huo pia umeweza kulipa hundi 49,467 na kati ya hizo 46,000 ni za pensheni za kila mwezi kwa wastaafu na 3,467 za madai mapya.
Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuhusu hati fungani, mifuko ambayo ilikuwa bado haijaridhia hati ya makubaliano kwa sasa zimesharidhia.
“Serikali inatarajia kutoa Hati Fungani ya Sh trilioni 2.6 yenye riba ya asilimia 6.5 kwenda PSPF. Hati fungani hizi zitaiva kwa vipindi tofauti, kuna za miaka mitatu, mitano, saba, 10 na kuendelea,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa miradi ya uwekezaji, Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT) kwa mujibu wa sheria ilikamilisha ukaguzi wa mifuko kwa mwaka 2015.
Ukaguzi huo ulisababisha mamlaka kwa kushirikiana na BoT kufanya ukaguzi maalumu kwenye majengo na milki za mifuko yote ya hifadhi ya jamii ukiwemo wa NSSF.
Aidha, ukaguzi huo unatarajiwa kuchukua kati ya miezi hadi tisa kulingana na upatikanaji wa taarifa na kwamba wakati kaguzi hizo zikiendelea mifuko iliyovuka viwango vya uwekezaji imezuiwa kuendelea kuwekeza katika maeneo hayo.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa mifuko imeonekana kuwa na gharama kubwa ya uendeshaji na kwamba kuwepo kwa gharama hizo kutazorotesha utendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
0 comments:
Post a Comment