Thursday, 14 April 2016

SHERIA ZA SOKA KUBADILISHWA KUANZIA MSIMU 2016/17!


 IFAB imetangaza mabadiliko ya Sheria za Soka ambazo yataanza kutumika kuanzia Msimu wa 2016/17 na kubwa ni ile inayohusu Wachezaji kupewa Kadi Nyekundu kwa Rafu ndani ya Penati Boksi.
IFAB, International Football Association Board, si FIFA, ndio yenye mamlaka pekee ya kutunga na kubadili Sheria za Soka.
Badiliko kubwa ni ile Sheria iliyompa Adhabu 3 kwa mpigo Mchezaji anaecheza Faulo kumzuia Mpinzani nafasi Dhahiri ya kufunga ambapo alikuwa akipewa Kadi Nyekundu, kusababisha Penati kutolewa dhidi ya Timu yake na kisha Mchezaji huyo huyo kufungiwa Mechi kwa kosa hilo hilo.
Sasa IFAB imeibadili Sheria hiyo ambayo Wachezaji watakaoonekana kufanya Faulo kwa bahati mbaya hawatapewa Kadi Nyekundu na badala yake wataonywa.
Lakini Wachezaji wanaowashika, kuwavuta au kuwasukuma Wapinzani, na wale wasiocheza Mpira au hawana nafasi ya kuucheza Mpira, wakifanya Faulo mbaya au kucheza vurugu au kuushika Mpira kwa makusudi, wao Adhabu yao iko palepale ya kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu.
+++++++++++++++++++++++++++++++++
IFAB:
-Ni International Football Association Board ambayo ina Wajumbe 8: FIFA hutoa Wanne na Nchi za England, Scotland, Northern Ireland na Wales (ambazo ndizo Nchi zonazohesabika kuanzisha mchezo wa Soka), hutoa Wajumbe 4.
+++++++++++++++++++++++++++++++++
Badiliko jingine la Sheria ni lile la kuwapa Marefa uwezo wa kumtoa nje Mchezaji yeyote hata kama Mpira haujaanza rasmi na hii huanzia pale Waamuzi wakiingia Uwanjani kuukagua Uwanja kabla ya Mechi kuanza.
Kingine ambacho kimebadilika ni ile Sheria iliyotaka Wachezaji wakiumizwa kwa Rafu iliyostahili Kadi ya Njano au Nyekundu kulazimishwa kutolewa nje ya Uwanja kutibiwa na kuwapa Wapinzani manufaa ya kucheza na Timu pungufu kwa muda.
Sasa, katika mabadiliko haya, Wachezaji walioumizwa katika mazingira kama hayo, watatibiwa Uwanjani na wataanza Mechi humo humo badala ya kutoka nje na kuomba kurudi.
Vile vile, IFAB imepitisha majaribio ya Miaka Miwili ya kutumia Teknolojia ya Video kuwasaidia Marefa kufanya maamuzi sahihi katika matukio ya aina 4.
Matukio hayo ni kuamua kama Goli limefungwa, Kadi Nyekundu, Penalti na pale wanapohitaji kuhakikisha kuwa Mchezaji sahihi anapatikana kwa kosa alilofanya.
Ikiwa majaribio haya yatafuzu basi huenda Teknolojia ya Video ikaanza kutumika kuanzia Msimu wa 2017/18.
Nchi 13 zimejipendekeza kufanya Majaribio haya ya Teknolojia ya Video kusaidia Marefa zikiwemo England na Scotland.

0 comments: