Saturday, 4 January 2014

MWILI WA DK MGIMWA WAWASILI NCHINI NA VILIO VYA ZIDI KUTANDA KWA TZ



Mke wa aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu William Mgimwa, Jeni(katikati) akifuta machozi jijini Dar es Salaam jana,baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere. Picha na Michael Jamson 


Dar es Salaam. Vilio, simanzi na majonzi, vilitawala jana katika Uwanja za Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, wakati mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Dk William Mgimwa, aliyefariki dunia Afrika Kusini, ulipowasili nchini.
Mamia ya wananchi wakiwamo viongozi mbalimbali wa Serikali na wanasiasa, jana walijitokeza uwanjani hapo kuanzia saa 4.30 asubuhi na ilipofika saa 7.45 mchana, ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), iliyobeba mwili huo ilitua uwanjani hapo.
Mjane wa marehemu, Jane Mgimwa akiambatana na watoto wake walishuka kutoka ndani ya ndege hiyo na kupokewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
Baada ya mwili huo kuwasili , msafara wa magari ulianza kuelekea nyumbani kwa marehemu Mikocheni B Mtaa wa Ruvu, jijini Dar es Salaam ambapo ibada fupi ya Misa Takatifu ilifanyika na baadaye mwili wa Dk Mgimwa ulipelekwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo kuhifadhiwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, Rais Jakaya Kikwete ndiye atakayewaongoza viongozi wa Serikali na wananchi kutoa heshima zao za mwisho kabla mwili haujapelekwa kijijini kwa marehemu, Magunga mkoani Iringa kesho.
Marehemu Dk Mgimwa, alifariki dunia Januari Mosi mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, iliyoko mjini Pretoria, alikokwenda kwa matibabu, zaidi ya mwezi mmoja na nusu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari, Januari 2 mwaka huu Waziri Lukuvi alisema, Serikali itaweka wazi chanzo cha kifo wakati wa kumuaga marehemu kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Hatuwezi kusema leo (Alhamisi, Januari 2 mwaka huu), hapa kwa sababu siyo busara. Hatujapokea hata taarifa ya daktari, nafikiri siku tutakayokuwa tukimuaga kwenye Viwanja vya Karimjee, ndipo tutapata nafasi ya kueleza hilo,” Lukuvi alinukuliwa akisema. 
Baada ya shughuli ya kuaga  mwili huo Viwanja vya Karimjee, utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini Magunga, kupitia Iringa mjini ili kuwapa nafasi wananchi kutoa heshima za mwisho, kisha kwenda kijijini ambako mwili huo utalala, kabla ya maziko yatakayofanyika kesho.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim alisema kuwa marehemu Dk Mgimwa atakumbukwa kwa utendaji kazi wake uliotukuka, ambapo kwa muda mfupi aliweza kuijengea heshima Wizara ya Fedha iliyokuwa imepoteza imani kwa wananchi.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib  Bilal, akisani Kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa, aliyefariki dunia Januari 01, 2014 huko nchini Afrika ya Kusini alikokuwa amelazwa kwa matibabu. Dkt. Bilal alifika kuhani msiba huo nyumbani kwa marehemu Mikocheni B, jijini Dar es Salaam, leo jioni. Picha na OMR 3.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimfariji mke wa marehemu Dkt. Mgimwa, Jane Mgimwa, wakati alipofika kuhani msiba huo nyumbani kwa marehemu Mikocheni B, jijini Dar es Salaam, leo jioni. Picha na OMR 4 5 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwafariji wanafamilia wa marehemu Dkt. Mgimwa, wakati alipofika kuhani msiba huo nyumbani kwa marehemu Mikocheni B, jijini Dar es Salaam, leo jioni. Picha na OMR
Baadhi ya Mawaziri na wabunge waliofika kuhani msiba huo nyumbani kwa marehemu Mikocheni B, Jana.

Related Posts:

0 comments: