Tuesday, 21 January 2014

MBWA YAGEUKA KUA MBOGA KUTOKANA UKAME NCHINI KENYA

110920121357 china dog meat 304x171 bbc nocredit1 6aa01Kisa cha kusikitisha kimeripotiwa kutokea katika jimbo la Turkana ambapo mwanamke mmoja mkongwe alilazimika kupikia familia yake nyama ya Mbwa kutokana na uhaba wa chakula unaokumba eneo hilo. 
Hali mbaya ya ukame imesababisha uhaba wa chakula na kuwalazimu baadhi ya wakaazi ambao ni wafugaji wa kuhamahama kula nyama ya Mbwa.
 
Tukio hilo limeripotiwa katika eneo la Kakuma ambapo akina mama wawili walipatikana wakikaanga kitoweo cha nyama ya Mbwa.

Chifu wa eneo hilo Cosmus Nakaya amethibitishia BBC tukio hilo ambapo, wanawake wawili walikamatwa katika eneo hilo ambalo ni hifadhi kwa maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia,wakikaanga kitoweo cha nyama hiyo tayari kuwalisha watoto.
Mama Akaran Aparo, mwenye umri wa miaka 73, aliambia maafisa kuwa alilazimika kupikia familia yake nyama hiyo kwani hakutaka kuiba Mbuzi au Kuku wa mtu kisha akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Aidha Mama Aparo aliwaambia waandishi wa habari kwamba yeye hulazimika kusafiri umbali wa kilomita 3 kutafuta chakula katika kambi ya Kakuma ingawa hurejea na kidogo sana au wakati mwingine kukosa hata hicho kidogo.
Mama huyo alisema kuwa yeye hutegemea chakula cha msaada kwani anaishi na wajukuu wake watano ambao wazazi wao walifariki.
Anasema yeye hupokea chakula cha msaada lakini hajapokea chochote tangu mwezi Septemba mwaka jana.
Jimbo la Turkana ni kame sana ingawa hivi karibuni kumekuwa na habari njema kutoka katika jimbo hilo kwani visima vya mafuta vimepatikana pamoja na visima vya maji vilivyo chini ya ardhi.
Utajiri huu unatarajiwa kuboresha maisha ya wenyeji ingawa hadi mavuno yatakapoanza kupatikana ndipo faida zitakapoanza kudhihirika kwa wenyeji wa jimbo hilo. Chanzo: bbcswahili

Related Posts:

0 comments: