* Asaini kitabu cha maombolezo ya Waziri Mkuu wa zamani
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametumua salamu
za rambirambi kwa Serikali ya Ireland kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri
Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Bw. Albert Reynolds.
Hayati Reynolds ambaye amefariki akiwa na
miaka 81, alikuwa Waziri Mkuu wa nane wa nchi hiyo kwa miaka mitatu
kuanzia mwaka 1992. Atakumbukwa kwa kuanzisha mchakato wa kuleta amani
Ireland Kaskazini dhidi ya kundi la IRA.
Waziri Mkuu Pinda ambaye aliwasili jana
(Alhamisi, Agosti 28, 2014) jijini Dar es Salaam akitokea Dodoma,
alikwenda moja kwa moja ubalozi wa Ireland na kusaini kitabu cha
maombolezo cha kiongozi huyo.
Katika salamu za rambirambi, Waziri Mkuu
amemwelezea Bw. Reynolds kuwa ni kiongozi atakayekumbukwa kwa kuleta
amani duniani na misaada ya kimaendeleo nchini Tanzania.
“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania,
ninawapa pole sana kwa kufiwa na Kaka yetu na ndugu yetu, Waziri Mkuu wa
zamani wa Ireland, Albert Reynolds. Tunashirikiana nanyi katika kipindi
hiki cha majonzi. Tutaendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri alizofanya kwa
nchi yetu na duniani. POLENI SANA KWA MSIBA HUU MKUBWA,” inasomeka
sehemu ya salamu za rambirambi alizotoa Waziri Mkuu.
Akipokea salamu hizo, Balozi wa Ireland
nchini Tanzania, Bibi Fionnuala Gilsenan alimshukuru Waziri Mkuu Pinda
kwa kufika ubalozini hapo na kuwapa pole kwa kifo cha Waziri Mkuu wao wa
zamani.
“Tutamkumbuka kiongozi wetu kwa mambo
mengi aliyoifanyia nchi yetu… Tunafarijika kwa salamu hizi za
rambirambi. Tutafikisha kitabu hiki cha salamu za rambirambi kwa familia
yake, naamini nao watafarijika sana,” alisema Balozi Gilsenan.
Balozi Gilsenan alimweleza Waziri Mkuu kwamba kitabu cha maombolezo kitafungwa leo.
0 comments:
Post a Comment