WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili kwa siku 10, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameibukia Kigali, Rwanda ambako michuano ya Kombe la Kagame inaendelea.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), yupo Kigali kwa siku tatu sasa na amekuwa akihudhuria mechi za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Uwanja wa Nyamirambo.
Hakuonekana kabisa uwanjani jana wakati Azam FC ikimenyana na Adama City ya Ethiopia na kushinda 4-1, lakini juzi na leo amefika Nyamirambo.
Akiwa kwenye eneo la ‘watu wazito’ maarufu kama VIP Uwanja wa Nyamirambo, Poppe ameonekana kudadisi wachezaji kadhaa wanaomvutia.
Mawindoni; Hans Poppe wa pili kulia akiwa Uwanja wa Nyamirambo APR na KCC zikimenyana |
Katika mchezo wa leo kati ya APR na KCC, Poppe aliinuka na kwenda kuulizia zaidi kwa mtu juu ya wachezaji Mwiseneza Djamal na Mugiraneza Baptiste wa timu ya jeshi la Rwanda.
Poppe aliulizia umri wa Djamal na baada ya hapo akatulia na kuendelea kuangalia mchezo- huku akionyesha dalili zote za kuwapiga hesabu wachezaji hao.
TFF imeongeza kwa siku kumi muda wa kumalizika usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutokana na kuchelewa kwa link ya mfumo mpya wa usajili (system) kutoka Shirikisho la Soka Miguu Afrika (CAF).
Kwa mujibu wa CAF, link hiyo itakuwa tayari kwa matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutokana sasa. Hivyo, mameneja wa usajili wa timu hizo kwa sasa wanatakiwa kukamilisha nyaraka zote zinazotakiwa ili link hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara moja.
Poppe akiwa bize Uwanja wa Nyamirambo leo |
Kuanzia msimu wa 2014/2015 mfumo unaotumika kwa usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa zamani wa kutumia fomu za kawaida. Mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na CAF unaondoa upungufu uliokuwepo katika mfumo wa zamani.
Kutokana na mabadiliko hayo, usajili sasa utamalizika Agosti 27 mwaka huu badala ya leo (Agosti 17 mwaka huu). Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Agosti 28 mwaka huu hadi Septemba 3 mwaka huu.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana kati ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia pingamizi na kuthibitisha usajili.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoshirikisha timu 14 itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia kutoka mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza inatarajia kuanza wiki ya kwanza ya Oktoba.
Mwisho wa kuombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba 6 mwaka huu.
Hata hivyo, Simba SC tayari ina wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, ambao ni mabeki Mganda, Joseph Owino, Mkenya, Donald Mosoti, Warundi kiungo Pierre Kwizera na Amisi Tambwe pamoja na mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera
Pamoja na hayo, kumekuwa na tetesi kwamba idadi ya wachezaji wa kigeni itaongezwa kutoka watano hadi saba.
Na Mahmoud Zubeiry, KIGALI
0 comments:
Post a Comment