Kaimu
Katibu Tawala wa wilaya ya Ngara Bw. Hussein Seif akitoa ufafanuzi kwa
wajumbe wa maandalizi ya shughuli ya uzinduzi wa Programu ya uimarishaji
wa mipaka ya Kimataifa wa wilaya ya Ngara itakayozinduliwa na Rais
Jakaya Kikwete eneo la Mugikomero mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Wanaoonekana nyuma ni raia wa Burundi waishio mpakani.
Raia
wa Burundi wakiwa nyuma ya alama ya mpaka inayotenganisha Tanzania na
Burundi. Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
inaendelea na zoezi la kuhuisha mipaka hiyo ya kimataifa.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete anatarajia kuwa
mgeni rasmi katika uzinduzi wa programu ya uimarishaji wa mipaka ya
kimataifa kwa lengo la kuhuisha alama zilizopo na kuweka mpya katika
maeneo ya mipaka ya Tanzania ambayo awali yalikuwa yametengwa na mito
na baadaye mito hiyo kukauka .
Programu
hiyo inayofanywa na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi itazinduliwa rasmi Agosti 28, katika eneo la mpaka kati ya
Tanzania na Burundi la Mugikomero wilayani Ngara mkoani Kagera kwa
upande wa Tanzania na eneo la Nteritare kwa upande wa Burundi.
Aidha,
itahusisha ujenzi na uwekaji wa vigingi vya mipaka, Marais wa nchi za
Burundi na Tanzania kutembelea baadhi ya maeneo yenye alama za mipaka na
kisha kuzungumza na wananchi waishio mpakani.
Katika
tukio hilo Rais Jakaya Kikwete anatarajia kumpokea mwenzake wa Burundi,
Rais Pierre Nkurunziza atakayewasili nchini Tanzania kushuhudia zoezi
hilo akitokea nchini Burundi kupitia mpaka wa Kabanga ulioko wilayani
Ngara.
Kaimu
Katibu Tawala wa wilaya ya Ngara Bw. Hussein Seif akizungumzia
maandalizi ya shughuli hiyo amesema kuwa wilaya hiyo imejipanga
kuhakikisha kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa ufanisi katika maeneo
yote ya wilaya ya Ngara yanayopakana na nchi ya Burundi.
Naye
Mkurugenzi Msaidizi wa Topographia na Giodosia wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. James Mtamakaya akizungumzia zoezi
hilo amesema kuwa tayari maeneo mbalimbali ya mipaka ya Tanzania
yameshapitiwa na zoezi hilo likiwemo eneo la mpaka kati ya Tanzania na
Uganda.
Ameyataja
maeneo mengine kuwa ni eneo la Tanzania na Rwanda ambalo bado
linatenganishwa na mto Rusumo, eneo la mpaka kati ya Tanzania na
Msumbiji, Tanzania na Kenya pamoja na zoezi la uimarishaji wa mpaka kati
ya Burundi na Tanzania ambalo linaendelea kufanyika.
Dkt.Mtamakaya
ameeleza kuwa zoezi hilo lina umuhimu katika kuhakikisha ulinzi na
usalama wa mipaka na kuongeza kuwa ni utekelezaji wa azimio la Umoja wa
Afrika (AU) kwa nchi wanachama kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2017 kila
nchi iwe imekamilisha programu hiyo.
Akizungumzia
changamoto wanazokutana nazo wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo amesema
ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi hususani raia wa pande zote ambao
wengi wao wamejenga ndani ya maeneo ya hifadhi ya alama za mipaka
ambayo kisheria hayaruhusiwi kujengwa kutokana na alama za mipaka
zilizowekwa na wakoloni kuwa umbali mrefu kutoka eneo moja hadi jingine.
“Baada
ya kuanza kwa zoezi la kuhuisha mipaka baadhi ya Raia wa Tanzania na
Burundi wamejikuta wamejenga ndani ya eneo la mpaka ambalo
haliruhusiwi jambo kinyume cha sheria za kimataifa, wengi wao
wamejenga kwenye maeneo hayo kwa kuvamia kutokana na mipaka iliyowekwa
na wakaoloni kuwa umbari mrefu nao kujikuta wamo eneo la nchi nyingine
lazima taratibu za kuwaondoa zifanyike ” Amesisitiza Dkt. Mtamakaya.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO
26/8/2014. Ngara, Kagera.
0 comments:
Post a Comment