Thursday, 28 August 2014

USAJILI LIGI KUU BARA WASOGEZWA MBELE KWA MARA NYINGINE TENA


DIRISHA la usajili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa wachezaji wazalendo limesogezwa mbele kwa Saa 48 kuanzia jana, kutokana na timu kushindwa kukamilisha usajili katika muda husika jana.
Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa amei uwambia mtandao huu leo kwamba, sababu za kusogeza mbele ni klabu zote za Ligi Kuu kushindwa kukamilisha usajili jana.
“Nadhani wameshindwa kuutumia huu mfumo wetu mpya wa elektroniki, sasa tumewapa Saa 48 zaidi warekebishe, zikiisha hizo, hapo hakuna nafasi tena, tunasonga mbele,”amesema Mwesigwa.


Amesema kwamba hadi muda wa kufunga usajili jana Saa 6:00 usiku, ni timu moja tu, Kimondo FC ya Daraja la Kwanza ndiyo iliyokuwa imefanikiwa kukamilisha usajili wake katika mfumo huo. “Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Kimondo kwa kumudu kuutumia mfumo huu na kuwasilisha usajili wao ndani ya muda,”amesema.
Aidha, Mwesigwa amesema kwamba dirisha la usajili kwa wachezaji wa kigeni litafungwa Septemba 6, mwaka huu. “Hili dirisha la wachezaji wa kigeni likifungwa, hakuna nyongeza ya muda tena, kwa kuwa hili lipo katika mfumo wa kimataifa chini ya FIFA, likifungwa, limefungwa dunia nzima, hivyo nawasihi viongozi wa klabu wahakikishe hawafanyi makoasa,”amesema. 


 Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM

0 comments: