Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
imekabidhiwa msaada wa vifaa vyenye thamani zaidi ya milioni mia moja
kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa ajili ya matumzi ya
ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Mambo ya ndani na ukumbi wa mikutano wa
Jeshi la Polisi Tanzania.
Msaada huo, ulitokana na Ziara ya
Naibu Waziri wa Usalama wa raia wa Jamhuri ya watu China aliyoifanya
hapa nchini mwezi mei mwaka jana ambapo aliahidi misaada mbalimbali kwa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi.
Miongoni mwa vifaa
vilivyokabidhiwa na Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini Mhe.
Xu Youqing kwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Pereira
Silima ni pamoja na Kompyuta Thelasini (30), Viti tisini na mbili (92),
Meza hamsini (50) na PA System kwa ajili ya kumbi mbili za mikutano.
Aidha, Balozi wa Jamhuri ya watu
wa China hapa nchini Mhe. Xu Youqing alikabidhi Pikipiki hamsini (50)
kwa Jeshi la Polisi ambazo zilipokelewa rasmi na Naibu Waziri wa Mambo
ya ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Silima.
Pikipiki hizo zilitolewa na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya watu wa China kwa niaba ya jumuiya ya
wafanyabiashara wa kichina walipo Afrika wakati wa ziara yake
aliyoifanya hapa nchini mwezi juni mwaka huu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo
ya Ndani ya nchi Mhe. Pereira Silima baada ya kupokea vifaa hivyo,
alimshukuru Balozi huyo wa China na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China
Pamoja na Wafanyabiashara wa Kichina waliopo Afrika kwa msaada
walioutoa kwa Serikali ya Tanzania, na kueleza kuwa vifaa hivyo vyote
vitakuwa ni chachu katika kuzuia, kupambana na kukabiliana na uhalifu
hapa nchini.
Naye, Naibu Inspekta Jenerali wa
Polisi, Abdulrahman Kaniki alisema kuwa mbinu za kutenda uhalifu
hubadilika mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia, na
katika kukabiliana na mabadiliko hayo Jeshi la Polisi liko kwenye
utekelezaji wa Maboresho yaliyojikita katika mihimili mikuu mitatu
ambayo ni kulifanya Jeshi kuwa kisasa, lenye weledi na linaloshirikiana
na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu, hivyo vifaa
vilivyokabidhiwa vitalisaidia Jeshi la Polisi katika mpango huo
unaolenga kuzuia uhalifu.
Na. Tamimu Adam – Jeshi la Polisi
0 comments:
Post a Comment