Mkurugenzi
wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey Mwakasyuka (kushoto) akitoa ufafanuzi
mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na malipo ya
posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo katika ukumbi wa mikutano
ofisi ya Bunge mjini Dodoma
Baadhi
ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wakisikiliza kjwa
makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey
Mwakasyuka wakati alipofanya mkutano na waandishi hao kwa lengo la
kutolea ufafanuzi kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba leo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini
Dodoma
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
26/08/2014.
OFISI ya Bunge Maalum la Katiba
mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo
vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba.
Ufafanuzi huo umetolewa leo na
Mkurugenzi wa Habari na Itifaki Bw. Jossey Mwakasiyuka wakati
alopokutana na waandishi wa habari kwa lengo la kutolea ufafanuzi
kuhusiana na taarifa hizo zilizoikera ofisi hiyo ya Bunge Maalum.
Mwakasyuka amevieleza vyombo vya
habari kuwa, ofisi ya Bunge Maalum imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa
hizo na baadhi ya vyombo vya habari kwani taarifa hizo ni za upotoshaji
na zina lengo la kuwadhalilisha Waheshimiwa Wajumbe na kuwafanya
waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa.
“Ni vema ikaeleweka kwamba Wajumbe
wa Bunge Maalum wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye
kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato na kwamba Ujumbe wa
Bunge Maalum ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia
taifa Katiba Mpya”. Alisema Mwakasyuka.
Mwakasyuka ameongeza kuwa, si vema
kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha Wajumbe hao kwa njia yoyote ile
kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya
kazi ya Bunge Maalum vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.
Akifafanua kuhusiana na malipo ya
posho hizo, Mkurugenzi Mwakasyuka ameviambia vyombo vya habari kuwa,
Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao wanahudhuria vikao vinavyoendelea
wamekwishalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.
“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo
ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye
mchakato maalum unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya Wajumbe
kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina, na upatikanaji wa fedha
toka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika.”
Alifafanua Mwakasyuka.
Aidha, Mwakasyuka
amevitahadharisha vyombo vya habari vinavyondika habari za Bunge Maalum
kuzingatia maadili na kanuni za Uandishi wa habari zinazotolewa katika
vikao vya Bunge Maalum ili taarifa kama hizo za upotoshaji zisijirudie
tena.
“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni
kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii
kutokana na uandishi usio makini”. Alionya Mwakasyuka.
Katika kanuni za Bunge Maalum,
kanuni ya 77 inawataka waaandishi wa habari kuandika habari za Bunge
Maalum kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari
ili kuondoa uandishi wenye kuleta chuki kati ya Serikali na Wananchi
wake kwani kinyume na kanuni hiyo, Katibu anaweza wakati wowote kuondoa
ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa chombo chochote cha habari iwapo
chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli za Bunge Maalum
ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au vinginevyo
inakiuka kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum.
0 comments:
Post a Comment