Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda
MATUKIO
ya kukata viungo vya walemavu wa ngozi (albino), yameendelea mkoani
hapa, ambapo juzi mlemavu wa pili katika muda usiozidi wiki mbili,
amekatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho
kusikojulikana.
Suzana
Mungi (35) ambaye ni mlemavu wa ngozi na mkazi wa Kijiji cha Buhelele
kata ya Nsimbo wilayani Igunga, amekatwa kiwiko cha mkono wake na
wahusika kutoweka nacho kusikojulikana.
Katika
tukio hilo lililofanyika juzi, mume wa Suzana, Mapambo Mashili ameuawa
kikatili kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati
akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.
Hivi
karibuni mtoto Upendo Sengerema (15), mkazi wa Kijiji cha Usinge, Kata
ya Uganza Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, alikatwa mkono na wahalifu
ambao walikimbia nao. Mpaka sasa Upendo amelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Urambo mkoani hapa.
Akizungumzia
tukio hilo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, alisema kitendo hicho ni cha
kinyama, ambacho hakiwezi kuvumiliwa na mtu yeyote.
Alisema
watu wote watakaobainika kufanya unyama huo, watachukuliwa hatua kali za
kisheria ili kukomesha vitendo hivyo visivyokuwa vya kistaarabu.
Aidha,
aliwataka wakuu wa wilaya zote mkoani hapa, kutambua maeneo yote ambayo
wanaishi walemavu wa ngozi na kuwa karibu nao kwa ajili ya kuimarisha
ulinzi wao kila siku katika maeneo wanayoishi.
Dau la RC
Mkuu wa huyo wa Mkoa, ametangaza dau la Sh 500,000 kwa mwananchi yeyote
atakayetoa taarifa za kupatikana kwa wahalifu wanaojihusisha na matukio
hayo.
Pia,
Mwassa aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Tabora, kuhakikisha waliofanya
matukio hayo, wanakamatwa na kutiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani
kujibu mashitaka yanayowakabili.
Kamanda
wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda, aliwataka wakazi wa Mkoa wa
Tabora, kuachana na imani za kishirikina na kueleza kuwa atahakikisha
wahusika wanakamatwa.
CHANZO:HABARILEO
0 comments:
Post a Comment