MCHAKATO wa kujadili na kuandika
Katiba Mpya unaendelea bungeni mjini Dodoma, licha ya kuwepo kwa mvutano
na mgawanyiko wa makundi ya wabunge wa bunge maalumu wanaojadili Rasimu
ya Pili iliyowasilishwa kwao. Wakati hayo yakiendelea viongozi,
wanaharakati na wadau wa watoto wanapendekeza masuala ya haki za msingi
za watoto yatambulike vizuri katika katiba ijayo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika
yanayofanya kazi na Watoto Tanzania ambaye pia ni Mratibu Miradi, Kituo
cha Watoto wa Mtaani cha Dogodogo Kigogo (Dogodogo Centre Street
Children Trust), Sabas Masawe anashauri ibara ya 43 ambayo inataja haki
za msingi za watoto iendelee kuwepo mpaka Katiba inakamilika na
iboreshwe zaidi katika mchakato unaoendelea Bungeni. Nasema haya maana
tayari kuna baadhi ya watu wameanza kuhoji kwamba kwanini hata watoto
wanaingia kwenye katiba ilhali wao ni sehemu ya watu kama wazazi wao.
Anasema pamoja na kuingizwa
kipengele cha mtoto kwenye rasimu ya pili ya katiba bado kuna mambo
ambayo wao kama wadau wangependa yaingizwe tena hivi sasa katika
mchakato wa majadiliano unaoendelea. Anasema baadhi ya mambo hayo ni
kama umri wa mtoto mwenyewe kutaja wazi kwamba ni kuanzia umri gani.
“…Unaweza ukaangalia hili ni suala
la msingi sana kutaja umri wa mtoto mwenyewe anayezungumziwa…kwa sisi
wadau wa watoto tunashangaa sana kwa maana nyingine tunaona suala hilo
ni kama linaongeza utata, kumuweka mtoto kwenye katiba ilhali umeshindwa
kumtambua (kiumri) mtoto ni yupi ni sawa na vichekesho…tunashauri mtoto
huyu umri utajwe wazi kuondoa utata…,” anasema.
Mfano ukisema wazee wana haki ya
kutibiwa bure lazima useme huyu mzee anaanzia umri gani na kuishia wapi.
Huwezi kusema wazee watibiwe bure alafu unashindwa kuainisha vitu vya
muhimu kama umri wao, bila hivyo utaleta mkanganyiko wa tafsiri…ndiyo
maana hata sasa mtoto anayetajwa tunataka tujue anaanzia umri gani na
kuishia umri gani. Sasa hili pekee linatushangaza watu wasomi wanajadili
bila kuliona hili.
Huyu mtoto akiingia kwenye
mgongano katika sheria anashughulikiwa namna gani kwasababu hili
linaweza kuwa na mgongano kama pia litashindwa kutajwa kwenye katiba
chombo ambacho ni sheria mama ya nchi. Masawe anasema mambo mengine
ambayo yanatakiwa kuainishwa ni pamoja na kuelekeza namna ya
kuwawajibisha wazazi ambao wamekuwa wakikimbia majukumu yao ya kulea
watoto na kuwapeleka katika vituo vya yatima eti kwa madai wamewashinda.
0 comments:
Post a Comment