Baadhi
ya washiriki katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa
za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara. Uzinduzi huo
umefanywa na mjane wa hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Taasisi ya Graca Michel Trust, Bi. Graca Michel leo jijini Dar es
Salaam.
Mjane
wa Hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca
Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel (kulia) akishangilia baada ya
kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu za viganjani kwa simu zote
zilizosajiliwa nchini Tanzania ikiwa ni ishara ya uzinduzi kampeni za
kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara.
Mjane
wa Hayati Nelson Mandela na Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust
(GMT), Bi. Graca Michel akimbusu mmoja ya watoto wa kike kutoka Mkoa wa
Mara kuonesha ishara ya upendo katika uzinduzi huo.
Mjane
wa Hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca
Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel akisalimiana na baadhi ya viongozi
mbalimbali kutoka mkoani Mara.
Baadhi
ya watoto wa kike kutoka Mkoa wa Mara wakizungumzia namna
walivyonusurika kufanyiwa vitendo vya kikatili (kukeketwa). Kulia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka akiwasikiliza.
Viongozi
mbalimbali wastaafu wa Serikali, viongozi wa dini Mkoa wa Mara,
wawakilishi wa wanafunzi Mkoa wa Mara wakiwa katika hafla ya uzinduzi
rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike
zitakazoendeshwa mkoani Mara.
Baadhi
ya viongozi wa mashirika mbalimbali walioshiriki hafla ya uzinduzi wa
kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa
mkoani Mara. Uzinduzi huo umefanywa na mjane wa hayati Nelson Mandela,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel Trust, Bi. Graca
Michel leo jijini Dar es Salaam.
Mjane
wa Hayati Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca
Michel Trust (GMT), Bi. Graca Michel (kulia) akizungumza kabla ya
kuzindua rasmi kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike
zitakazoendeshwa mkoani Mara.
Baadhi
ya wanafunzi wakiangalia ujumbe mfupi uliotumwa kwa simu zote
zilizosajiliwa kwa njia ya simu za kiganjani na Mjane wa Hayati Nelson
Mandela, Bi. Graca Michel kwa kushirikiana na Waziri wa Maendeleo ya
Jamii Jinsia na Watoto, Bi. Sophia Simba kupinga ndoa za utotoni kwa
watoto wa kike.
Baadhi ya wanafunzi wakitumbuiza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike.
Moja
ya kikundi cha maigizo kikionesha igizo namna mtoto wa kike
anavyokabiliana na changamoto za unyanyasaji kutoka kwa jamii katika
hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za kupinga ndoa za utotoni kwa watoto
wa kike
JUMLA ya wasichana wenye umri
mdogo wapatao 984 wameolewa na kukatishwa masomo huku wasichana wengine
1,628 wakikeketwa wilayani Tarime, Mkoa wa Mara ikiwa ni miongoni mwa
vitendo vya kikatili ambavyo amekuwa akifanyiwa mtoto wa kike baadhi ya
maeneo nchini Tanzania.
Takwimu hizo za vitendo vya
kikatili dhidi ya mtoto wa kike wilayani Tarime zimetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele kwa niaba ya
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa kampeni za
kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike zitakazoendeshwa mkoani Mara.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa
kampeni hiyo, Henjewele alisema takwimu hizo zavitendo vya kikatili
Mkoani Mara ni za kuanzia mwaka 2013 hadi Juni 2014. Alisema baadhi ya
familia eneo hilo wanamchukulia mtoto wa kike kama kitega uchumi hivyo
wamekuwa wakiwaozesha mapema ili kupata mali (yaani ng’ombe) jambo
ambalo bado uongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na wadau anuai wamekuwa
wakipinga na kupambana na ukatili huo.
“…Matukio ya vitendo vya
unyanyasaji kwa mtoto wa kike kwa mwaka 2013 hadi Juni 2014 ni kama
ifuatavyo; watoto wa kike wapatao 984 waliozeshwa, wasichana 1,628
walikeketwa, jumla ya wanafunzi wa kike 4,134 walipewa mimba na
kukatishwa masomo yao huku wasichana 1,912 wakifanyiwa ukatili wa vipigo
kwenye familia ama kwenye ndoa na jumla ya watoto 11 walibakwa…,”
alisema Henjewele.
Aidha alisema vitendo hivyo vya
kikatili kwa mtoto wa kike vinachangiwa na baadhi ya jamii mkoani humo
kuendeleza mila na desturi zilizopitwa na wakati, migogoro ya koo,
mwamko duni wa elimu kwa jamii na usiri mkubwa wa kutokubali mabadiliko
dhidi ya vitendo vya kikatili kwa jamii hiyo. Akizungumzia jitihada
zinazofanywa na viongozi wilayani hapo kukabiliana na vitendo hivyo,
alisema wamekuwa wakiendesha semina na vikao mbalimbali na wazee wa
kimila, mangariba na jamii kwa ujumla kwa lengo la kutokomeza vitendo
vya Ukatili wa kijinsia, ukeketaji pamoja na mila na desturi zilizopitwa
na wakati.
Kwa Upande wake mjane wa hayati
Nelson Mandela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Michel
Trust, Bi. Graca Michel akizungumza kabla ya kuzindua rasmi kapeni hizo
alisema viongozi kwa kushirikiana na wanajamii mkoani Mara wakiamua kwa
dhati wanaweza kukabiliana na ndoa za utotoni na vitendo vingine vya
kikatili eneo hilo.
Akizungumzia kwa ujumla alisema
jamii nyingi ya kiafrika bado zinamthamini mtoto wa kiume zaidi ya yule
wa kike ilhali watoto wote wanapaswa kuwa na haki sawa. Aliwataka wazazi
wenye mawazo kama hayo kubadilika na kutoa haki sawa kwa watoto bila
ubaguzi. Alishauri suala la uamuzi dhidi ya maisha ya mtoto lifanywe kwa
ushirikiano kwa familia nzima pamoja na kushirikishwa mtoto.
“…Lazima tukubali kubadilika,
umefika wakati suala la uamuzi wa wakati gani wa kuolewa kwa mtoto wa
kike ufanywe kwa ushirikiano kati ya wazazi wote pamoja na mtoto
mwenyewe tena kwa wakati muafaka…lazima turejeshe maamuzi pia kwa mtoto
mwenyewe si kutumia nguvu kwa kila kitu,” alisema Bi. Michel.
Aliongeza hata hivyo ipo haja ya
kuwa na asasi za ushauri ngazi ya familia ambazo zitakuwa zikitoa
ushauri juu ya masuala ya familia kwa kuzingatia sheria na taratibu
zinazotambulika. Alisisitiza katika kampeni za sasa juhudi na elimu ya
kutosha itolewe kwa jamii mkoani Mara ili baadaye ifanyike tathmini kwa
eneo hilo jambo ambalo linaweza kusaidia mapambano maeneo mengine hapo
baadaye.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA,
Valerie Nsoka akifafanua juu ya shughuli za kampeni hizo alibainisha
kuwa zitaambatana na utoaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo
viongozi wa dini, watendaji wa vyombo vinavyosimamia sheria, viongozi wa
jamii na jamii kwa ujumla juu ya mapambano ya kampeni hizo. Kampeni
hizo baadaye zitaendelea katika maeneo mengine ya Tanzania.
Programu ya kampeni hiyo
imefanikishwa kwa kushirikiana na Serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa
la Idadi ya Watu (UNFPA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Shirika
lisilo la Kiserikali la Children’s Dignity Forum (CDF), Graca Machel
Trust (GMT), asasi za mkoani Mara na uongozi wa mkoa.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
0 comments:
Post a Comment