Tuesday, 19 August 2014

JK AKUNA KICHWA KUFANYA MAAMUZI NDANI YA CCM KATIKA KAMATI KUU LEO DODOMA. ;



  Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM inakutana leo mchana mjini Dodoma chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete huku ikitarajiwa kufanya uamuzi mgumu wa mchakato wa Katiba.

Kikao hicho kinaketi mara ya pili katika muda mfupi, baada ya hivi karibuni kukaa jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na mchakato huo.


Hata hivyo, safari hii kikao hicho kinaketi kukiwa na maswali lukuki ambayo hayajapata majibu: Je, Bunge la Katiba liendelee au livunjwe? Je, lisitishwe kwa muda kupisha maridhiano au la? Je, kuna umuhimu wa maridhiano? Kuna ulazima wa kuwapo Ukawa bungeni?


Akizungumzia kikao hicho, mtaalamu wa sayansi ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema jambo kubwa litakalojadiliwa katika kikao hicho ni kauli tofauti zilizotolewa na wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya.




“Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba ameshauri yafanyike maridhiano kwanza na wapo wanaCCM waliomuunga mkono. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema naye ameonyesha wasiwasi wake, Ukawa na Jukwaa la Katiba Tanzania nao wamesema yao. Nadhani kuna jambo CCM wameliona na wanataka kuliweka sawa,” alisema Dk Makulilo.


Aliongeza, “Kujua nini wataamua ni ngumu lakini kutokana na hali ilivyo kwa sasa ni wazi kuwa wanakutana kuona nini kifanyike.”


Kwa upande wake Bashiru Ali alisema, “Tangu mwanzo mchakato wa Katiba haukuwa katika ilani ya CCM, sasa unaweza kujiuliza wanakwenda kujadili nini wakati hata katika mikakati yao ya miaka 10 na 20 ijayo hakuna mpango wa kuandika Katiba.”


Habari zilizozagaa mjini Dodoma zinadai kikao hicho pia kinaweza kupendekeza kuwashughulikia wanachama wake waliotoa kauli zinazopingana na msimamo wa chama hicho.


Miongoni mwa waliotoa kauli zinazopingana na chama hicho ni Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba kutokana na matamshi yake ya kuhoji uhalali wa vikao vya Bunge la Katiba kuendelea bila uhakika wa akidi.


Mbali na Mwigulu pia wabunge kadhaa wa CCM akiwamo, Esther Bulaya (Viti Maalumu), Kangi Lugora (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa), Ridhiwani Kikwete (Chalinze) nao wamekaririwa kwa nyakati tofauti wakitoa misimamo inayokinzana na chama chao kuhusu uhalali wa Bunge la Katiba kuendelea bila kuwapo maridhiano na Ukawa.


Hata hivyo, habari nyingine zinasema iwapo kuna mpango huo, Mwigulu anaweza kuondolewa kutokana na utaratibu wa chama hicho kuwaondoa kwenye sekretarieti wajumbe wake wanaoteuliwa kushika nyadhifa serikalini.


Chanzo chetu kinasema ikiwa hilo litatokea kwa sababu ya Mwigulu kuteuliwa Naibu Waziri wa Fedha, basi mpango huo hautamwacha nyuma Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dk AshaRose Migiro ambaye pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba.


Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na gazeti hili jana, alikanusha kuwapo kwa mpango wa kumwondoa Nchemba katika nafasi yake na kwamba kikatiba kikao chenye uwezo huo ni Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.


“Hizo taarifa ni za uongo kabisa, kikao kweli kitakutana kesho (leo) saa 8:00 mchana chini ya Mwenyekiti Rais Kikwete na ajenda ni moja tu, ambayo ni mchakato wa Katiba. Kikao maalumu huwa na ajenda moja maalumu, hakuna mengineyo wala nini,” alisema Nnauye.


Alisema CC itapokea taarifa kuhusu mchakato wa Katiba unavyokwenda itakayotolewa na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro na baadaye kujadiliwa na wajumbe.


Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana zinasema hatua dhidi ya kiongozi huyo wa juu katika chama zinatokana na kile kinachoelezwa kuwa ni “kuwaudhi makada wa CCM” kutokana na kauli yake hiyo.


Nchemba jana alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kupitia ujumbe mfupi wa maandishi, “Sina taarifa za kung’olewa, nimealikwa kwenye kikao kama NKM (Naibu Katibu Mkuu wa CCM).”


Hata hivyo, ikiwa CCM itafanya uamuzi wa kumwondoa Nchemba, huenda ukapokewa kwa hisia tofauti na umma wa Watanzania ikizingatiwa kwamba pamoja na kutoa kauli zinazokinzana na msimamo wa chama chake, amekuwa akiungwa mkono na wananchi wa kada mbalimbali.


CC ya CCM ambayo hivi karibuni ilibariki Bunge la Katiba kuendelea hadi lifike mwisho, inakutana leo kwa dharura wakati mchakato wa Katiba ukidaiwa kutokuwa na uhalali wa kisiasa kutokana na kususiwa na idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Kutokana na kutokuwapo Ukawa ndani ya Bunge, kuna hofu kwamba Bunge linaloendelea na vikao vyake Dodoma litakosa theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar, hivyo kutopatikana Katiba Mpya.


Kutokana na hali hiyo, Mwigulu amekaririwa mara kadhaa akisema hakukuwa na haja ya Bunge hilo kuendelea na vikao bila kuwa na uhakika wa kutimiza akidi, vinginevyo itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma, na wananchi hawatawaelewa.


Kutokana na mazingira hayo, vyanzo vya habari vinasema CCM lazima ifanye uamuzi mgumu wa ama kuziba masikio isisikie kelele za makundi yanayotaka Bunge lisitishwe hivyo iamue liendelee, au igeuke jiwe kwa kulisitisha na kukiuka uamuzi wake wa awali.


Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa kwamba viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakifanya vikao vya siri na wale wa vyama vya upinzani kwa lengo la kufanyia marekebisho Katiba ya sasa ili kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi mkuu mwakani iwapo Katiba mpya itakwama.


Miongoni mwa maeneo ambayo vyama hivyo viliyaainisha katika vikao vyake vya siri ni pamoja na kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, matokeo ya kura za Rais kuhojiwa mahakamani na mgombea binafsi.

0 comments: