Saturday, 23 August 2014

TAARIFA KUHUSU ZIARA YA WAZIRI MKUU UWANJA WA NDEGE MWANZA.


images
Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Pinda kesho, Jumamosi Agosti 23, 2014 anatarajiwa kukagua ujenzi wa kiwanja wa Ndege wa Mwanza unaopanuliwa miundombinu na majengo ili kuwezesha ndege kubwa za safari za mizigo zinazolingana na BOEING 747 (CODE D to CODE E) kutua na pia kuhudumia abiria zaidi ya milioni 2 katika jengo jipya la abiria. Waziri Mkuu atakuwa mkoani hapa Mwanza kwa ziara ya kiserikali kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kushiriki kama mgeni rasmi katika shughuli za BWM Foundation.. Uwanja wa ndege wa Mwanza unapanuliwa kwa gharama ya sh,. Bilioni 105. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania inatoa sh. Bilioni 85 na benki ya BADEA na Shirika la OFID kwa pamoja (sh. Bilioni 20) zikiwa ni mkopo. Maeneo ambayo Waziri Mkuu, Mh. M.K. Pinda anatarajiwa kukagua ni jengo la kuongozea ndege (control tower), njia ya kurukia na kutua ndege inayorefushwa kwa mita 500 zaidi kutoka mita 3,300 za sasa ili kuwezesha ndege kubwa za mizigo za Boeing 747 kutua na kuruka katika uwanja huo bila matatizo. Eneo lingine litakalotembelewa na Waziri Mkuu ni la mtambo wa lami (asphalt plant) itakayozalisha lami inayotumika kujenga barabara inayorefushwa ya kuruka na kutua ndege.Mtambo huu unamilikiwa na mkandarasi wa mradi huu, kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ya China. Mhandisi Mshauri wa mradi huo ni Kampuni ya United Engineering and Technical Construction (UNETEC) ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) inayofanya kazi ya usanifu na usimamizi wa mradi kwa gharama ya dola za Marekani 3,376,031.00. Akiwa uwanjani hapo katika ziara itakayoanza saa 3.00 asubuhi kesho, Jumamosi, Waziri Mkuu, Pinda anatarajiwa kupata taarifa ya maendeleo ya mradi huo wa ujenzi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wanaojenga miundombinu hiyo ya usafiri wa anga. Kazi ya ujenzi ilianza Julai 2012 na mkataba wa kazi na mkandarasi ulisainiwa Juni 2012. Awali muda wa kumaliza kazi ulipangwa uwe miezi 24 , yaani mwishoni mwa mwaka huu 2014 lakini kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali sasa kazi itamalizika Oktoba 2015.. Kazi zinazofanyika mpaka sasa ni urefushaji wa njia ya kurukia ndege na kutua, upanuzi wa maegesho ya ndege za abiria, ujenzi wa jengo la abiria na miundombinu yake(barabara ya kuingia na kutoka kwenye maegesho).

Nyingine ni ujenzi wa jengo la mizigo, ,maegesho ya ndege za mizigo, jengo la kuongozea ndege, kituo cha umeme, maegesho ya magari , mifumo ya maji ya mvua na mifumo wa maji safi na taka kwa ajili ya kiwanja kizima. Ujenzi huu utakapokamilika utaufanya uwanja wa ndege wa Mwanza kuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa nchi za maziwa makuu na kuwezesha ndege za kimataifa (intercontinental flights) kutua. Pia utaongeza uwezo wa jengo la abiria kuhudumia abiria na mizigo kutoka abiria 500,000 kwa mwaka hadi abiria milioni 2 kwa mwaka. Upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010. TAA inasimamia viwanja 58 yya ndege vya serikali, inajenga vipya na kuendeleza vilivyopo ambapo hivi sasa inaendelea na ujenzi wa jengo la tatu la abiria kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyrere (JNIA), Dar Es Salaam, lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka. Jengo hilo la kisasa linajengwa na mkandarasi, BAM International ya Uholanzi na linatarajiwa kukamilika Oktoba 2015. Aidha, TAA imekamilisha miradi kadhaa ukiwemo wa kiwanja cha ndege cha Mpanda, Mafia na cha Songwe, Mbeya.
IMETOLEWA NA GODFREY JOHN LUTEGO AFISA UHUSIANO – OFISI YA SHERIA NA UHUSIANO TAA (TEL. O713-507777)

0 comments: