WATU sita
wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika matukio mawili
tofauti yaliyoambatana na mvua katika mikoa ya Mwanza na Kagera.
Katika
tukio la jijini Mwanza, vilio na simanzi jana vilitawala kwa wakazi wa
maeneo ya Sinai-Mabatini, baada ya vifo vya watu wanne wa familia mbili
tofauti, vilivyotokana na mvua iliyosababisha miamba mikubwa ya mawe
kuporomoka na kuponda nyumba zao usiku wa manane.(Martha Magessa)
Tukio
hilo la kusikitisha limeripotiwa kutokea saa nane usiku kuamkia jana,
wakati mvua iliyoambatana na upepo wa wastani ilipokuwa ikiendelea
kunyesha, na kuababisha miamba hiyo mikubwa inayokadiriwa kufikia tani
mbili kuporomoka na kuziponda nyumba hizo na kusababisha vifo hivyo na
majeruhi wanne.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua.
MTANZANIA
Jumapili lilifanikiwa kufika eneo la tukio na kushuhudia miamba hiyo
ikiwa imeharibu nyumba, huku nyumba moja iliyojengwa kwa matofali ya
tope ikiwa imeanguka na kubaki kifusi.
Nyumba
zilizokumbwa na maafa hayo zinamilikiwa na watu waliotajwa kwa majina ya
Joseph William na Lameck Ajiji, na kila moja watu wawili wamefariki kwa
kukandamizwa na miamba hiyo.
Katika
nyumba ya William iliyokuwa na watu watano, waliofariki wametajwa kuwa
ni Kefa Joseph (15) na Emmanuel Joseph (12), wote mwanafunzi wa Shule ya
Msingi Mbugani na majeruhi mmoja ambaye hakufahamika jina lake ambaye
alikimbizwa hospitali.
Nyumba
inayomilikiwa na Ajiji yenye watu watatu, waliofariki wametambuliwa kuwa
ni mama wa nyumba hiyo, Kwinta Geko (24) na mumewe Samson Odinya.
Waliojeruhiwa ni mtoto Bety Samson (4) na Godfrey Joseph (14) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani.
Tukio
hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo la Sinai. Mara ya kwanza
ilikuwa ni mwaka 2009 baada ya miamba kuporomoka na kusababisha vifo vya
watu wawili wa familia moja.
Tukio la jana lilivuta hisia tofauti kwa wakazi wa Jiji la Mwanza, huku wengine wakiangua vilio.
Mamia ya wananchi waliofika eneo hilo, walijitolea kwa kumpa fedha mtoto Bety aliyenusurika kufa kutokana na tukio hilo.
Mbunge wa
Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (Chadema), alifika eneo la tukio
na kutoa pole kwa wananchi, ndugu jamaa na marafiki wa familia
zilizoathirika na janga hilo, ambapo alionyesha kushtuka baada ya
kuelezwa na wananchi kwamba hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyefika
eneo hilo.
Akizungumza
kwa kutumia kipaza sauti mbele ya umati wa watu waliokuwa wamefurika
katika eneo hilo la tukio, alisema: "Inashangaza sana kuona hata mkuu wa
wilaya hajafika hapa. Nitawasiliana na viongozi wa Serikali na mchana
nitarudi hapa tena."
Baadhi ya
wananchi waliozungumza na MTANZANIA Jumapili katika eneo la tukio,
waliiomba Serikali kuzuia wananchi kujenga karibu na miamba mikubwa,
kwani kufanya hivyo itasaidia sana kuepusha maafa kama hayo.
"Kwa
kweli tukio hili linasikitisha sana, na tunaomba viongozi wa serikali
wasaidie wananchi kuwaondosha kwenye maeneo ya kwenye miamba," alisema
mmoja wa wananchi hao ambaye pia ni balozi wa Shina Namba Tano, Mtaa wa
Nyerere A, Jackson Kitundu.
Katika
tukio jingine, watu wawili wa familia mojawakazi wa Kitongoji cha
Kaburi, Kata ya Kanoni wilayani Karagwe, wamefariki dunia papo hapo na
wengine watatu kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, amethibisha tukio hilo na
kusema lilitokea juzi mchana baada ya mvua kubwa kunyesha ikiambatana na
upepo mkali pamoja na radi.
Waliofariki
dunia wametajwa kuwa ni Coletha Porotas (30) na Onesimo Nestori (14),
huku waliojeruhiwa ni Emmanuel Jeremia (44), Tumsifu Emmanuel (10) na
Jovinus Nestori (10), wote wakazi wa Kitongoji cha Kaburi, Kijiji cha
Kanoni, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Akizungumzia
tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kaburi, Willison Kristian,
alisema mvua hiyo iliyonyesha kwa takribani saa moja, iliambatana na
mawe, upepo mkali na radi.
Kristian alisema radi hiyo iliwakuta watu hao ndani nyumba tofauti katika kijiji hicho na kuwarusha nje
CHANZO:MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment