Wednesday, 12 February 2014

RAISI KIKWETE :MARUFUKU KUUZA HAZINA YA VIPUSA VYA TEMBO VILIVYO KAMATWA

Rais Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabango ya kuhamasisha wananchi kupiga vita mauaji ya Tembo na Farubaada ya kuyazindua rasmi kwenye  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Tanzania Limited, Juma Pinto. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Dk. Mahamoud  Mgimwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Said  Meck Sadick.
Rais Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabango ya kuhamasisha wananchi kupiga vita mauaji ya Tembo na Farubaada ya kuyazindua rasmi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Tanzania Limited, Juma Pinto. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Dk. Mahamoud Mgimwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadick.

RAIS Jakaya Kikwete, amesema Tanzania haitauza nje shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa katika matukio mbalimbali nchini, ambayo yamehifadhiwa.

Amesema yuko tayari kuamuru meno hayo yachomwe moto iwapo hayatakuwa na kazi mbadala lakini si

kuuzwa. Amesema hatatoa kibali cha kuuzwa meno hayo ili kusaidia harakati za kukabiliana na ujangili nchini.

Alisema hayo juzi usiku, alipozindua mabango ya kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika vita dhidi ya ujangili, akiwa njiani kwenda London, Uingereza, ambako leo atahutubia kwenye mkutano maalumu kuhusu kupambana na ujangili wa tembo.

Mkutano huo umeitishwa na mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles, ambapo viongozi wa mataifa zaidi ya 50 duniani watahudhuria, Rais Kikwete akiwa kiongozi wa kwanza kuhutubia.

Alisema miaka kadhaa iliyopita Tanzania ilifanikiwa kupambana na wimbi la ujangili lakini mambo yameharibika kutokana na kurejea kwa biashara ya meno ya tembo, ambayo vinara wa ununuzi ni mataifa makubwa.
“Tumewahi kukumbwa na majanga makubwa ya ujangili mara mbili, awamu ya kwanza ilikuwa miaka ya 70 hadi 1980. Wakati wa Uhuru tulikuwa na tembo zaidi ya 350,000 lakini walipungua hadi kufikia 50,000.” 
Kutokana na hilo, alisema mwaka 1989 serikali iliingiza jeshi katika Operesheni Uhai na mikakati mbalimbali ya kupambana na ujangili, ambapo mafanikio makubwa yalipatikana.

Alisema hadi mwaka 2009 idadi ya tembo iliongezeka maradufu na kufikia zaidi ya 150,000 lakini sasa imeanza kuwa mbaya kutokana na kushamiri kwa ujangili.

Kuhusu faru, ambao wanakabiliwa na tishio la kutoweka kwa kasi, alisema mwaka 1989 walibaki wawili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambapo wote walikuwa majike kabla ya kuingia dume kutoka Hifadhi ya Ruaha na kuanza kuzaliana.
“Sasa tuna faru 32 na tumeingia kwenye rekodi ya faru wanaozaliana kwa haraka duniani.”
Alisema kuendelea kwa ujangili kunatokana na kuwepo soko la meno ya tembo na nyara nyingine.

Rais Kikwete alisema jitihada za ndani pekee haziwezi kuwa na mafanikio makubwa, hivyo ni lazima mataifa mengine yahusishwe.
“Nakwenda London kwa mazungumzo ambayo yalianza mwaka jana, yakilenga kufunga masoko ya meno ya tembo na faru. Nitakwenda kuwaambia wazungumze na wenzao kukomesha biashara ya meno ya tembo”
Alitaja masoko makubwa ya meno ya tembo kuwa, Thailand, Vietnam na China na kwamba, yakifungwa ujangili utakuwa historia.

Rais Kikwete alisema pia kumeanza kushamiri biashara ya ngozi za simba, chui na wanyamapori wengine, ambayo inatishia ustawi wa wanyama hao nchini.

Awali, akizungumza kabla ya kuzinduliwa mabango hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alisema lengo ni kuchochea ushiriki wa Watanzania katika kupambana na ujangili.

--- Imeandikwa na Rabia Bakari/gazeti la Uhuru

Tanzania haitauza meno ya Tembo

Pascal Shelutete, TANAPA

Related Posts:

0 comments: