Mgombea ubunge wa Chadema kalenga Grace Tendega baada ya kuruhusiwa gari lake kupita |
Hapa polisi wakimtazama mgombea huyo akipita mbele yao |
|
Diwani Nyalusi kati akiwa chini ya ulinzi wa polisi |
Diwani wa Chadema kata ya Mvinjeni Iringa mjini Frank Nyalusi wa pili kushoto akiwa chini ya ulinzi wa polisi leo |
Viongozi wa Chadema Iringa wakiwa na mgombea wa ubunge jimbo la Kalenga katikati Bi Grace T Mvanga |
mgombea wa Chadema jimbo la Kalenga Grace T Mvanga akizungumza na wanahabari leo baada ya kuchukua fomu |
JESHI la polisi mkoani Iringa leo
limeuzuia kwa muda msafara wa mgombea ubunge jimbo la Kalenga
kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Grace Tendega
Mvanga kwa madai kufanya maandamano yasiyo na kibali.
Huku Polisi hao wakimshikilia kwa
muda diwani wa kata ya Mivinjeni Frank Nyalusi ( Chadema) kwa madai
ya kuandaa mapokezi hayo bila kibali .
Tukio la kuzuiwa kwa mgombea huyo
lilitokea mida ya saa 5 asubuhi wakati msafara wa mgombea huyo
ukiwa na magari zaidi ya matano na pikipiki zaidi ya 20 ukikaribia
kuingia Samora katika mji wa Iringa .
Hata
hivyo mbali ya msafara huo kuzuiwa zaidi ya dakika 20 katika eneo
hilo Mlima wa Ipogolo barabara kuu ya Iringa- Dodoma polisi
waliweza kutumia busara zaidi ya kumruhusu mgombea wao kupita
kuelekea kuchukua fomu huku wafuasi wengine wakizuiliwa kwa
dakika tano na kuruhusiwa kumfuata mgombea wao ili kuufanya msafara
huo kuwa katika hali ya kawaida na sio maandamano kama ilivyokuwa
awali.
Pamoja na kuwaruhusu wafuasi hao ambao
baadhi yao walianza kutoa lugha ya matusi kwa askari hao na
kuwalazimisha kufyatua risasi jambo ambalo askari hao polisi
hawakuweza kufanya hivyo wala kuwapiga mabomu ya machozi zaidi ya
kumchukua kiongozi wao Frank Nyalusi kwa mahojiano zaidi.
Akizungumzia hatua ya polisi kuzuia
msafara huo kwa muda katibu wa Chadema wilaya ya Iringa vijijini
Felix Nyondo alisema kuwa wameshangazwa na hatua ya polisi kuzuia
msafara huo kwani hayo hayakuwa maaandamano bali ni mgombea wao
kutoka nyumbani kwenda kuchukua fomu kwa mujibu wa utaratibu wa
msimamizi wa uchaguzi huo.
Nyondo alisema walivyofanya Chadema
ni kama walivyofanya CCM wakati mgombea wao akienda kuchukua fomu
ambapo CCM walikwenda mbali zaidi kwa kuwa na watu ambao walikuwa
wakitembea kwa miguu na wao Chadema hawakufanya hivyo na badala
yake walitumia magari na pikipiki kuelekea kwa msimamizi huyo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa
Ramadhan Mungi alipotafutwa kwa njia ya simu na mtandao huu wa
www.matukiodaima.com ili kuelezea zaidi hatua ya kuzuia msafara huo
na kumshikilia kada huyo wa Chadema hakuweza kupatikana japo mmoja
kati ya maofisa wa polisi waliokuwepo eneo la tukio alisikika
akisema kuwa lengo la kuzuia msafara huo halikuwa lina ubaya ila ni
katika polisi kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha kila kitu
kinafanyika kwa misingi ya sheria.
Kwani alisema Chadema walipaswa
kuomba kibali kwa ajili ya kumpokea na kumsindikiza mgombea wao
kuchukua fumu na polisi wangekuwepo kwa ajili ya kulinda usalama wao
ikiwa ni pamoja na kuwaongoza njia ambavyo wangependa kupita ila
sio hivyo walivyofanya kwa kutumia nguvu kusababisha msongamano wa
magari katika barabara hiyo.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa
Chadema kalenga Bi Mvanga akizungumza na wanahabari alisema kuwa
anawapongeza wana Chadema jimbo la kalenga kwa kuendelea kumuunga
mkono na kuwa lengo la Chadema ni kuona wana Kalenga wanampata
mrithi wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Dr Wiliam Mgimwa
(CCM) mwenye uwezo wa kuwatumikia wananchi ambapo kwa upande wake
anao uwezo huo.
Mgombea huyo alipongeza shughuli
mbali mbali za kimaendeleo zilizofanywa na mbunge Dr Mgimwa kwa jimbo
la kalenga na kuahidi kuendeleza jitihada hizo za kimaendeleo iwapo
wananchi wa Kalenga watamchagua katika uchaguzi huo mdogo.
" Kuna mambo ambayo marehemu aliahidi
na kuishia njiani katika kuyafanikisha na kuwa nafasi hiyo
ataitumia kwa kufuatilia yote ambayo hayajafikia ukingoni "
Kuhusu msafara wake kuzuiwa na polisi
alisema kuwa hizo ni changamoto za kuwaida katika kuelekea kwenye
ukombozi wa kweli kwa wana kalenga kumpata kiongozi makini .
Zoezi
la uchukuaji fomu la mgom bea huyo lilifanyika majira ya saa sita
mchana katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi Jimbo la KalengaPudenciana
Kisaka ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halimashauri ya Iringa Vijijini.
Kisaka
alimkabidhi fumo namba 8 mgombea huyo pamoja na nyaraka mbalimbali za
Tume ya uchaguzi ikiwamo sheria za uchaguzi Kanuni za uchaguzi na pia
katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtaka mgombea kwenda
kujisomea kwa lengo la kuongeza uelewa ili kuepusha vurugu wakati wa
kampeni na uchaguzi wenyewe.
Kisaka
aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi sasa ni wagombea wawili kutoka
vyama vya CCM na Chadema pekee ndio wamejitokeza kuwania kiti cha
Ubunge katika jimbo hilo huku akiongeza kuwa mwisho wa kurejesha fomu ni
Februari 18 mwaka huu .
“Hadi
sasa tunavyama viwili ambavyo wagombea wake wameshachukua fomu ya
kuwania Ubunge kwa jimbo la Kalenga ,hata hivyo sheria bado inatoa Fursa
kwa vyama kuendelea kujitokeza hadi kuchukua na kurejesha hadi leo
kabla ya saa kumi jioni”alisema Kisaka.
Uchaguzi
wa Kalenga unatarajia kufanyika Machi 16 mwaka huu na unalengo la
kuziba pengo lililoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Marehemu
Dk Wiliam Mfimwa aliyefariki dunia Januari Mosi mwaka huu,katika
uchaguzi huo CCM imemsimamisha Godfrey Mgimwa mmoja w awatoto w marehemu
Mgimwa kupeperusha bendara ya chama hicho.
Grace
T Mvanga alipata kugombea jimbo la Kalenga kwa mara ya kwanza
mwaka 2005 kupitia Chama cha Jahazi Asilia na kushika nafasi ya pili
kwa kura 13000 huku mgombea wa CCM kwa kipindi hicho George Mlawa
akishinda kwa kishindo na bila kukata tamaa mwaka 2010 Grace T.Mvanda
alijitokeza tena kugombea kupitia chama cha Jahazi Asilia na
kushuka kwa kupata kura 3000 pekee huku mgombea wa CCM Dr Wiliam
Mgimwa akiongoza na safari hii kuibukia Chadema ambao anagombea kwa
mara ya kwanza kupitia Chadema na mara ya tatu katika Historia yake ya
kuusaka ubunge Kalenga hivyo macho na masikio ya wengi kuona kama
atapanda ama atazidi kushuka zaidi
0 comments:
Post a Comment