Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua athari za mafuriko katika kijiji cha Fufu wilayani Chamwino, Dodoma, Januari 17, 2014.Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rehema nchimbi na kulia kwake ni Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akikagua daraja ambalo lilizibwa na maporomoko ya maji yaliyoambatana na magogo , mawe na udongo na kusababisha mafuriko katika kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa januari 17,20134. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua athari za mafuriko
yaliyokikumba kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa Januari 17, 2014.
Kulia kwake ni Naibu Waziri wa
Viwanda na Biashara na Mbunge wa Mpwapwa, Gregory Tewu na kushoto kwa
ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa,, Alfred Msovella. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
..........................
*Amtaka Meneja TANROADS apitie upya maeneo korofi
*Amtaka Meneja TANROADS apitie upya maeneo korofi
*Aahidi mabati 780, mifuko 2,600 ya saruji
kwa
walioathirika
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametembelea
vijiji vya Chipogoro na Fufu katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino, mkoani Dodoma
na kukagua maeneo mbalimbali ambayo yaliathiriwa na mafuriko kutokana na mvua
kubwa zilizonyesha kati ya Januari 2 hadi Januari 11, mwaka huu.
Akiwa katika kijiji cha Chipogoro
tarafa ya Rubi, Waziri Mkuu alikagua kituo cha polisi na nyumba zilizobomolewa,
choo cha zahanati na kukagua eneo la barabara inayojengwa ya kutoka Dodoma hadi
Iringa katika eneo lenye matatizo ya makaravati kuziba.
Kwenye kijiji cha Fufu katika
tarafa ya Makangwa ambacho kiko umbali wa kilometa 30 kutoka Chipogoro, Waziri
Mkuu alikagua maeneo ya makazi yaliyoathiriwa kwa mafuriko na kukagua baadhi ya
nyumba zilizobomoka kabla ya kuzungumza na wananchi na kuwapa pole.
Akizungumza na wakazi wa vijiji hivyo
leo (Ijumaa, Januari 17, 2014),
mara baada ya kupokea taarifa za maafa ya mafuriko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Meneja
wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu kuhakikisha anasimamia wakandarasi
wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake bado haujakamilika na kuainisha maeneo korofi
ili yafanyiwe marekebisho haraka.
“Nimekagua matundu katika daraja
moja pale Chipogoro na kuona ni madogo, mtaalamu anasema uchafu ulioziba ndiyo
umesababisha maji yasipite. Mimi si mhandisi na hizi ni mvua za kwanza tu, sasa
yakija maji mengi zaidi ya haya hali itakuwaje?, alihoji Waziri Mkuu.
“Hata hapa Fufu, kuna mahali
nimeona maji yanaonyesha yalikuja kwa kasi kubwa lakini upenyo wa kuingia
kwenye makaravati na kutokea upande wa pili ni mdogo sana... barabara hii ni
mkombozi lakini kama haitazingatia uhalisia wa maeneo itakuwa ni balaa,”
alionya.
Alimtaka pia awasimamie wakandarasi
hao ili wanapoweka matoleo ya maji wahakikishe upande wa pili barabara maji
hayo yanakwenda kwenye mikondo ya mto na siyo kuyaacha tu yasambae kiholela na
kuishia kwenye makazi ya watu au mashamba yao.
Waziri Mkuu aliahidi kutoa mifuko
ya saruji 2,600 na mabati 1,560 ambapo kila kijiji kitapata mifuko 1,300 na
mabati 780 ili kuwasaidia wakazi waliobomolewa nyumba zao waweze kujenga nyumba
za kisasa.
Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Dk. Rehema Nchimbi kuwashirikisha wadau wengine katika mkoa huo ili waone
wanawezaje kuchangia upatikanaji wa mabati mengi zaidi kwa ajili ya nyumba
zilizoezuliwa.
Kuhusu chakula cha msaada, Waziri
Mkuu alimtaka Dk. Nchimbi aandae makisio ya mahitaji ya chakula yaliyopo na
kuyafikisha Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna Idara inayosimamia maafa ili
waletewe chakula hicho haraka kwa sababu kipo.
Alisema anakubaliana na ushauri
uliotolewa kuhusu suala la ujenzi wa mabwawa ya kukinga maji ya mvua ili
kupunguza kasi ya maji yanayoporomoka kutoka milimani lakini akasema Serikali
imeanza na ujenzi wa Bwawa la Kidete lililoko wilayani Kilosa tangu yaliyopotokea
mafuriko wilayani humo.
Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya
Mpwapwa, Bw. Alfred Msovella, alisema nyumba 129 zilibomoka, vyoo 78 vimebomoka
kikiwemo cha zahanati ambapo wakazi 1,390 wamepoteza vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula,
magodoro, vyombo vya ndani na mifugo.
Bw. Msovella ambaye pia ni Mkuu wa
Wilaya ya Kongwa alisema hivi sasa, wakazi hao wanahitaji mahema 400, magodoro
381, madaftari ya wanafunzi na dawa za matibabu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Bi. Fatma Salum Ally akitoa
taarifa mbele ya Waziri Mkuu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
uwanja wa shule ya msingi Fufu, alisema jumla ya nyumba 26 zilibomolewa na mali
kama vyakula, samani, vyombo vya nyumbani na bidhaa za biashara kuharibika.
Alisema eneo la kijiji cha Fufu ni
tambarare na liko chini ya safu za milima na maji ya mvua yanayoporoka kutoka milimani,
huondoka polepole. “Hata hivyo, hali hii ya mafuriko imechochewa na ujenzi wa
barabara kuu kwa kiwango cha lami ambapo tuta la barabara mpya na vidaraja vidogo
vilivyowekwa vimekuwa kizuizi cha maji mengi yanayotoka milimani na hivyo
kuongeza tatizo la mafuriko,” alisema.
Mikutano hiyo ilihudhuriwa na Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Gregory Teu ambaye pia ni mbunge wa Mpwapwa
pamoja na mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde.
(mwisho)
0 comments:
Post a Comment