BAADHI
ya wazazi nchini wametakiwa kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye
ulemavu kwani kufanya hivyo ni kinyume cha haki za binadamu. Akizungumza
kwa njia ya simu na Fullshangwe, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya
Kibaha, Pwani, Regina Mbaji alisema wandishi wanapaswa kufanya kazi ya
ziada katika kuwaibua watoto wa aina hiyo popote walikofichwa. Alisema
kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto hao kutokana na
mtazamo hasi, wakizani kuwa na mtoto kama huyo katika familia kuwa ni
aibu na kioja wakati sio kweli.
Mbaji alisema jamii inapaswa
kutambua kuwa watoto wenye ulemavu ni binadamu kama wengine na wanahaki
sawa na wengine. “Kuna baadhi ya familia ambazo zimekuwa zikiwanyanyapaa
watoto au watu wenye ulemavu kwa kuwalaza wakati mwingine kwenye vyumba
vya mifugo kwa kweli huu ni unyama uliyopitiliza naviomba vyombo vya
habari kwenda mbali katika majukumu yao kwa kuibua unyama huu hususan
maeneo ya vijijini,”alisema Mbaji.
Mbaji alisema maeneo ya vijijini
bado wazazi wanaendelea kuwakosesha mahitaji ya msingi watoto hao,
ikiwemo elimu, wakidhani kuwa hawana uwezo wa kuelewa masuala mbalimbali
watakayofundishwa. Alitoa wito kwa jamii kuwafichua watoto hao popote
walipofichwa ili serikali iweze kuwapatia mahitaji yao kama wanayoyapata
watu wengine wenye viungo kamili.
0 comments:
Post a Comment