Tuesday, 7 January 2014

WATU WAWILI WAKAMATWA NA COCAINE NA VIPUSA VYA TEMBO

Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam linawashikilia watu wawili, Salma Omari (mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam) na raia wa China ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, kwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya cocaine pamoja na meno ya tembo.

Watu hao walikamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mmoja akiwa amevaa vipusa vya
tembo kiunoni kama urembo huku mwingine akiwa amemeza tembe za dawa za kulevya.

Watu hao walikuwa wakijiandaa kupanda ndege ya shirika la Ethiopian Airlines kuelekea nchini China kabla ya kushitukiwa na maafisa wa JNIA.

Walipopelekwa kwa uchunguzi katika hospitali ya Temeke, bi. Salma alikutwa na tembe 67 za cocaine tumboni ambapo mpaka jana jioni tayari alikuwa ametoa tembe 24.

Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani punde taratibu zitakapokamilika.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliyekuwa amefanya ziara ya kushitukiza uwanjani hapo alisema Serikali imedhamiria kukomesha uhalifu huo na itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote yenye mianya ya kupitisha dawa za kulevya na nyara za Serikali kwa magendo.

 

0 comments: