Waziri wa Ujenzi, John Magufuli akisisitiza jambo fulani siku za hivi
karibuni, yeye ndiye mwenye dhamana na nyumba za Serikali. Picha na
Maktaba
Dar es Salaam . Viongozi wa
Serikali wakiwamo mawaziri, wameingia kwenye kashfa inayowaweka katika
wakati mgumu, baada ya kubadili matumizi ya nyumba za Serikali
walizonunua, kinyume na mikataba inavyoeleza.
Nyumba hizo ambazo zilianza kuuzwa mwaka 2002 enzi
ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ziliuzwa kwa
mawaziri, makatibu wakuu na watumishi wengine wa ngazi mbalimbali za
umma.
Mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za
Serikali inaeleza kuwa, mfanyakazi wa Serikali anaponunua au kukopeshwa
nyumba, hatakiwi kubadili matumizi au kuuza hadi baada ya miaka 25
kupita.
Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na
10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba
hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka ishirini na mitano (25), kuanzia
tarehe ya hatimiliki.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Ujenzi, John
Magufuli mwenye dhamana na nyumba za Serikali kwa muda wa miezi miwili
kutoa ufafanuzi wa suala hilo bila mafanikio, huku akitoa sababu
mbalimbali kwa mwandishi kukwepa kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson
Lwenge alisema kuwa anahitaji kupata ripoti kamili kutoka kwa Wakala wa
Nyumba za Serikali (TBA), ili ajionee mikataba na afahamu ni wapi
ilipovunjwa.
“Serikali ina nia nzuri kabisa kuwauzia watumishi
wake nyumba, lakini kama kuna mikataba inakiukwa, basi TBA inafahamu kwa
kina ni kwa vipi watu hao wachukuliwe hatua,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, viongozi
wengi ambao nyumba zao zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na
Mwanza wamezibadili matumizi na kuwa za biashara.
Kwa Jiji la Dar es Salaam baadhi ya nyumba
zilizouzwa kwa vigogo hao wa Serikali na kubadilishwa matumizi zipo
katika maeneo ya Oysterbay.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya nyumba hizo
zikiwa zimebadilishwa matumizi na kuwa klabu za starehe, kupangishwa
taasisi au balozi, huku nyingine zikiwa tayari zimeuzwa.
Moja ya nyumba hizo ni ya aliyewahi kuwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohamed Seif Khatib,
iliyopo Oysterbay, Mtaa wa Bongoyo katika Barabara ya Hillpark. Nyumba
hiyo kwa sasa imevunjwa na kujengwa klabu na baa iitwayo Ocasa.
Alipoulizwa kuhusu nyumba hiyo na mkataba wake
unavyosema, Khatib alisema kwamba hajavunja sheria yoyote kwa sababu
hajauza nyumba hiyo.
Na Florence Majani, Mwananchi GAZETI
Na Florence Majani, Mwananchi GAZETI
0 comments:
Post a Comment