LONDON, ENGLAND
FACEBOOK, WhatsApp, Instagram na Twitter, ndiyo
mitandao inayotawala kwenye simu za viganjani za watumiaji wengi wa
huduma hiyo kwa sasa duniani, ukiweka kando mitandao mingine ya kijamii
kama Circle, Viber, Skype, Tango mingineyo.
Kwa watumiaji wa kawaida, hii ni burudani kubwa
sana kwao. Lakini jambo hilo limewaingiza kwenye gharama kubwa wanasoka
maarufu kwenye Ligi Kuu England kwa sababu wamewekewa mipaka ya matumizi
ya mitandao hiyo ya kijamii.
Kiungo Mghana, Emmanuel Frimpong, anayekipiga
kwenye kikosi cha Arsenal amejiweka kwenye hatari ya kukumbana na adhabu
kali baada ya kutuma picha kwenye Instagram inayomdhihaki kocha wa
Manchester United, David Moyes baada ya kufungwa na Sunderland kwenye
nusu fainali ya Kombe la Ligi.
Kwenye picha hiyo, Frimpong amemwonyesha Moyes
kuwa maisha ya Old Trafford yamemshinda na kuamua kurudi Goodison Park,
ambapo kocha huyo anaonekana akiwa ameshika ubao ulioandikwa ‘Goodison
Park’ maskani ya klabu yake ya zamani, Everton, aliyokuwa akiinoa.
Hata hivyo, Frimpong, alichukua muda mfupi sana
kuiondoa picha hiyo kwenye ukurasa wake baada ya kugundua kwamba
itamsababishia hasara kubwa ya kupigwa faini na klabu yake ya Arsenal,
Ligi Kuu England pamoja na Chama cha Soka cha England (FA).
Matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook na
Twitter imewawatia hasara mastaa wengi kwenye Ligi Kuu England kutokana
na kutozwa faini kali za pesa, huku baadhi wakiingia kwenye matatizo
zaidi kwa kutozwa hadi Pauni 2,000 kwa kila neno waliloandika.
Staa Michael Chopra alipigwa faini ya Pauni 15,000
na klabu yake ya Blackpool baada ya kuandika ujumbe kwenye Twitter
ulioponda programu za mazoezi za klabu hiyo.
Lakini, Chopra hakuwa mchezaji wa kwanza kupoteza
pesa kutokana na matumizi ya Twitter, kwenye orodha hiyo baadhi yao wamo
wachezaji wenye hadhi kubwa kwenye Ligi Kuu England; Ashley Cole, Rio
Ferdinand na Darren Bent. Makala hii inazungumzia wanasoka nyota ambao
walipoteza mamilioni ya pesa kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii
ya Facebook na Twitter.
Chopra apunwa Pauni 15,000
Straika huyo akiwa hajafunga bao lolote tangu
alipojiunga na Blackpool kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Ipswich
mwaka jana, amejikuta kwenye matatizo baada ya kutuma ujumbe kwenye
Twitter unaokosoa vifaa vya mazoezi vya timu hiyo na kudai kwamba kuna
wachezaji sita tu walio makini kikosini.
Kitendo hicho kimeikera klabu hiyo kwa sababu
ameonyesha dharau kubwa na hivyo kumpiga faini ya pesa hizo ambazo si
kiwango kidogo kwake.
0 comments:
Post a Comment