>>USIRI ULIGUBIKA UHAMISHO TOKA SANTOS!
>>MWANACHAMA BARCA AIBURUZA KLABU MAHAKAMANI IFUNGUKE!
JAJI
wa Mahakama huko Spain amekubali kusikiliza Madai dhidi ya Rais wa
Barcelona Sandro Rosell kuhusu Gharama halisi za Uhamisho wa Neymar
kutoka Santos ya Brazil.
Mwezi Juni Mwaka Jana, Neymar
alitambulishwa kama Mchezaji mpya wa Barca kwa Uhamisho wa Dau la Euro
Milioni 57.1 lakini kuwepo kwa Makubaliano ya kuweka Vipengele vya
Uhamisho huo kuwa siri vilizuia kutangazwa kwa kila kitu kuhusu biashara
iliyofanyika.
Sasa Jaji huyo atasikiliza Kesi ya awali
ili kuamua kama kulikuwepo na ukiukwaji wa Sheria kufuatia Malalamiko
ya Mwanachama wa Barca, Jordi Cases.
Waendesha Mashitaka wa Spain
wamekubaliana na Madai ya Mwanachama huyo wa Barca kwamba kulikuwepo na
ukiukwaji wa Sheria kwa kutumia Mkataba Feki.
Pia, wametaja Kitita cha Euro Milioni 40
kilicholipwa kwa Kampuni ya Baba yake Neymar ambacho hakikutangazwa
katika Uhamisho huo.
Juzi Jumatatu, Gazeti maarufu huko Spain, El Mundo, lilitoboa
kuwa Dau halisi la kumnunua Neymar ni Euro Milioni 95 kitu ambacho
kilimfanya Rais Sandro Rosell atake nafasi Mahakamani ili atoe ushahidi
na kujisafisha.
Hiyo Jumatatu, Rosell, akiongea na
Wanahabari alitamka: “Kuna vitu viwili nataka kusema. Kwanza Neymar
aligharimu Euro Milioni 57.1. Na hili nimesema mara nyingi. La pili, ni
ombi, kwa heshima namuomba Jaji aniite ili nitoe ushahidi na kumwambia
kila kitu anachotaka kujua kwa sababu hamna cha kuficha!”
Katika kuisikiliza Kesi hii, Jaji Pablo
Ruz anatarajiwa kukusanya taarifa toka kwa Neymar, Santos na Barcelona
kabla hajamwita Rosell aende mwenyewe Mahakamani kutoa Ushahidi.
0 comments:
Post a Comment