Mbunge wa Ubungo (Chadema) John Mnyika
Mbunge wa Ubungo (Chadema) John Mnyika, amerudia kauli yake ya kumtaka Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, kujiuzulu kutokana na tatizo la maji kujirudia katika jiji la Dar es Salaam.
Aidha pamoja na Profesa Maghembe kuondoka aliwataka wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka ya Maji na Kampuni ya Maji Jijini (Dawasa na maji Dawasco) watoe maelezo ya sababu za matatizo ya maji kurejea tena jijini.
Katika taarifa yake aliyoitoa jijini jana pia aliwataka wahusika hao wajieleze kwa umma ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais asiwachukulie hatua kwa uzembe.
Alikumbusa kuwa ni zaidi ya nusu mwaka umepita tangu Waziri Maghembe atoe ahadi za kurekebisha tatizo la maji lakini ameshindwa kusimamia utekelezaji wake na kumtaka kujiuzulu.
“ Iwapo Profesa Maghembe hatajiuzulu nitaeleza hatua zaidi ambazo nitachukua,”Alisema Mnyika.
Alizitaka Dawasa na Dawasco kurejesha huduma ya maji ndani ya wiki moja hasa maeneo yaliyokuwa yanapata mgawo.
Akizungumzia viongozi hao wa mamlaka kuchukuliwa hatua alisema wanastahili adhabu kwa kuisababisha hasara kwa serikali, kuathiri uchumi wa taifa na maisha ya wananchi waliokosa maji mara kwa mara ambayo ni huduma ya msingi ya binadamu na malighafi muhimu ya uzalishaji.
Taarifa ya Mnyika, ilikumbusha kuwa Februari mwaka jana aliwasilisha hoja binafsi kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji Dar es Salaam na kupendekeza Bunge kuingilia kati ili kuisimamia serikali kuchukua hatua za haraka.
“Iwapo hoja hiyo ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji Dar es Salaam yangekuwa yamepungua katika maeneo kutokana na hatua nilipendekeza zichukuliwe.”
“Hata hivyo, badala ya kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingesaidia kurekebisha udhaifu uliokuwepo na kumrejeshea imani kwa umma Waziri Maghembe aliondoa bungeni,”ilisema taarifa yake.
Mbunge wa Ubungo alisema baada ya Bunge Waziri Maghembe alizungumzia masuala ya maji Dar es Salaam; kupitia mikutano ya CCM akiwa kata ya Goba pia alizitaja akiwa kwenye mkutano na wafanyakazi wa Dawasa na Dawasco na kueleza hatua za haraka ambazo angesimamia katika kushughulikia tatizo hilo.
Mnyika alisema serikali haikuchukua hatua hivyo alitangaza kuongoza maandamano ya wananchi Machi 16 2013 kwenda Wizara ya Maji ili kupata majibu na kuisimamia serikali kuchukua hatua za haraka.
“ Hata hivyo maandamano hayo yalizuiliwa na Jeshi la Polisi kwa sababu zisizo za msingi na kuombwa kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani,”iIlisema taarifa ya Mnyika
Alisema maandamano hayo yangefanyika na hatua kuchukuliwa matatizo yangepungua tofauti na ilivyo sasa, hivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Pereira Silima, anapaswa kueleza umma lini rufaa hiyo itashughulikiwa maandamano yaweze kufanyika wananchi wapate majibu ya hatua za haraka nilizopendekeza ndani na nje ya Bunge.
Alizitaka mamlaka ya maji na kampuni ya maji jijini kuhakikisha kwamba katika kipindi kisichozidi wiki moja huduma za maji zinarejea katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata huduma hiyo kwa mgawo.
SOURCE:
NIPASHE
11th January 2014
0 comments:
Post a Comment