Waziri wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe
Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Kilimanjaro Airports Development (KADCO), imepanga kuufanyia ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akitoa taarifa kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa KADCO, Bakari Murusuri, alisema ukarabati huo pia utawezeshwa kufanywa kutoka Taasisi ya Misaada iitwayo Orio Grant Facility ya Uholanzi.
Alisema kati ya fedha hizo sehemu itakuwa msaada na sehemu itakopwa na serikali ya Tanzania kwa mkopo wa masharti nafuu.
Alisema fedha hizo zitatumika kukarabati njia ya kurukia na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara ya viungio na uboreshaji wa jengo la abiria ili kukabiliana na ongezeko la abiria.
Alisema mradi huo unatarajia kuanza katikati ya mwaka ujao na utakamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
Alisema mradi huu wa ukarabati wa uwanja kwa sasa upo katika awamu ya kwanza na awamu ya pili itaanza Juni, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, alisema mapato makubwa ya kiwanja yanatokana na tozo katika utuaji wa ndege pamoja na malipo yanayotozwa kwa abiria.
“Tangu KADCO ikabidhiwe kuendesha kiwanja cha KIA mapato yamekuwa yakiongezeka kwa wastani kila mwaka kutokana na ongezeko la kibiashara.
“Ongezeko hilo la kila mwaka ni wastani wa shilingi za Kitanzania bilioni moja toka Sh. bilioni 1.4 mwaka 1999 hadi kufikia Sh. bilioni 12.9 kwa mwaka 2012,” alisema.
Alisema sambamba na ongezeko hilo, KADCO imekuwa mlipaji mkubwa wa kodi mkoani Kilimanjaro na hutunukiwa tuzo mbalimbali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ulipajii mkubwa wa kodi mbalimbali za kisheria, pamoja na uzingatiaji wa sheria za ulipaji kodi hizo.
Alitoa mfano wa mwaka 2013 KADCO imekuwa mshindi wa tatu wa mlipa kodi mkubwa mkoani Kilimanjaro.
Alisema kutokana na mapato hayo kampuni imeweza kuendesha shughuli zake pamoja na ulipaji wa madeni kwa ufanisi.
Akizungumzia changamoto mbalimbali alisema kuongezeka kwa vitendo vya usafirishaji wa dawa za kulevya ndani na nje ya nchi imekuwa ni changamoto katika ulinzi na usalama wa uwanja.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa askari polisi wanaotakiwa kulinda mitambo yenye ya kuongezea ndege pamoja na eneo la kuongezea ndege yaani mnara wa kuongezea ndege na lango kuu la kuingilia uwanjani.
SOURCE:
NIPASHE
11th January 2014
0 comments:
Post a Comment