unnamed (1)
Na Edwin Moshi, Makete
Kufuatia kijiji cha Ndulamo wilaya ya Makete mkoani Njombe kukumbwa na janga la upepo mkali na kuezua nyumba 10 pamoja na jiko la shule ya msingi Ndulamo Jumamosi Februari 15, mkuu wa wilaya ya Makete kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali na wananchi wamefanya mkutano wa hadhara kijijini hapo kupata ufumbuzi wa janga hilo.
Mkutano huo uliofanyika leo kijijini hapo umewahusisha wananchi wote wa kijiji hicho ambao wamejitoa kwa hali na mali kuhakikisha janga hilo lililokikumba kijiji hicho linattuliwa kwa pamoja.
Akiongea kwenye mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro amesema janga hilo haliwezi kutatuliwa na serikali pekee bali ushirikiano wa pamoja baina ya serikali na wananchi ukiunganishwa pamoja utasaidia kuwasaidia wananchi wote waliopatwa na janga hilo.
unnamed (2)
Amesema kwa taarifa zilizopatikana kutokana na janga hilo zinaonesha kuwa nyumba 10 pamoja na jiko la shule ya msingi Ndulamo zilizokuwa zinakaliwa na kaya 8 zenye watu 34 ziliezuliwa pamoja na baadhi ya miti ya mbao na ya kuni iliyokuwa jirani na kitongoji cha kwa yuta kilichoathirika zaidi
Matiro amesema kamati ya ulinzi na usalama ilitembelea eneo lililopata janga hilo Februari 16, na kujionea athari zilizotokea ambapo walilazimika kuitisha mkutano wa hadhara uliofanyika hii leo
Mkazi wa kijiji hicho Juma Mahenge akizungumza kwenye kikao hicho amesema wao kama wananchi wameguswa na janga hilo na kupendekeza ipitishwe harambee kila mwananchi aliyehudhuria kutoa mchango wake na kitakachopatikana kielekezwe kwa wahanga.
unnamed (3)
“Mimi napendekeza wananchi tutoe kila tulicho nacho, iwe fedha, mbao, matofali, na pia kijiji hiki kina mafundi basi tuwaombe wajitolee kujenga nyumba hizo bure ama kama watahitaji fedha kidogo basi michango hii itumike kuwalipa mafundi hao” alisema Mahenge
Katika mkutano huo wamekubaliana kila kitongoji cha kijiji hicho kichangie ujenzi wa nyumba zilizobomoka na kila kijiji kimepewa nyumba za kuzihudumia, Msitu wa kijiji pamoja na miti iliyoanguka ipasuliwe mbao kwa ajili ya waathirika, na mafundi walioko kijijini hapo wasaidie katika ujenzi wa nyumba zilizobomoka ambapo kila fundi alikabidhiwa nyumba ya kujenga
Aidha ilifanyika harambee kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo ambapo jumla ya sh. 940,000/= zilipatikana katika harambee hiyo, na pia mfuko wa jimbo utasaidia kununua mabti kwa wathirika, ikisaidiwa na mchango kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
Wakati huu ambapo jitihada zikiendelea wananchi waliopatwa na janga hili wanahifadhiwa na ndugu na jamaa katika kijiji cha Ndulamo, na mkuu wa wilaya amesema kuwa wanatarajia ndani ya wiki mbili wananchi hao watakuwa wameshapata makazi yao.
unnamed