Monday, 27 January 2014

WATU WAWILI WAFARIKI DUNIA IRINGA




RPC Mungi 

NA DIANA BISANGAO WA , IRINGA
Watu wawili wafariki dunia mkoani Iringa katika matukio matatu tofauti likiwemo la mkazi wa kijiji cha Mkombwe kata ya Mafinga tarafa ya Ifwagi wilaya ya Mufindi bibi Tunu Mohammed (105) kuungua na moto wa kibatari chumbani kwake.
Akizungumza na mtandao huu  ofisini kwake leo Kamanda wa polisi mkoani Iringa Ramadhani Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 23 januari majira ya saa 5:45 usiku.
 
Kamanda Mungi alisema chanzo cha moto huo ni baada ya kibatari alichokuwa akitumia bibi Tunu kuangukia kitandani na kuanza kuunguza mashuka na blanketi huku yeye akiwa usingizini.
 
Wakati huohuo huko maeneo ya pori la kijiji cha Msuluti kata ya Magulwila tarafa ya Mlolo wilaya ya Iringa mtu mmoja mwanaume Method Nyemba (17) mchunga ng’ombe alikutwa amefariki baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya mti.
 
Kamanda Mungi alisema tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 24 januari majira ya saa 2:30 asubuhi ambapo marehemu alikutwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya miguuni, chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika.
 
Mbali na matukio hayo mawili, Kamanda Mungi alisema askari polisi wakiwa doria huko maeneo ya Igumbilo kata ya Ruaha manispaa ya Iringa waliwakamata raia wawili wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Mungi alisema tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 24 januari majira ya saa 2 kamili usiku ambapo aliwataja majina yao ni Tagas Awali (29) pamoja na Disele Ayeno (25), watuhumiwa hao wapo kituo cha polisi Iringa Mjini kwa mahojiano Zaidi.

0 comments: