*Wadaiwa kukata nondo za gereza na msumeno
WAFUNGWA
watatu wa gereza la Songwe wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani hapa, wametoroka
katika mazingira yenye utata wakiwa ndani ya sero ya gereza hilo.
Tukio hilo
la kushangaza, lilitokea kati ya Januari 14 na 15, mwaka huu, ambapo wafungwa
hao inadaiwa kuwa walikata nondo za dirisha la sero walimokuwemo kisha kuruka
na kutokomea kusikojulikana.
Taarifa za
uchunguzi, zimebaini kuwa, wafungwa hao walikata nondo hizo kwa kutumia msumeno
bila kubainika na askari waliokuwa kazini siku hiyo.
Taarifa zinasema
kuwa, wafungwa hao ni wakazi wa wilaya za Mbeya na Chunya ambapo mmoja wao
alikutana na Kamanda wa polisi wa wilaya ya Chunya, alipoulizwa kuwa ametokaje
gerezani, alimwambia kamanda huyo kuwa alitoka kwa msamaha wa Rais.
Mkuu wa magereza mkoa wa Mbeya SACP, Julius Sanguti,
amethibitisha kutoroka kwa wafungwa hao.
“Ni kweli
lakini ni mapema mno kulizungumzia tukio hilo kwasababu tunaendelea na
uchunguzi kwa kushirikiana na wenzetu wa jeshi la Polisi’’ alisema Sanguti.
Alipoulizwa
kama kuna askari anashikiliwa kwa uzembe na kama ana taarifa waliko wafungwa
hao, alisema hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kwa sasa kwasababu wanafanya uchunguzi.
‘’Ndiyo
maana nimekuambia kuwa ni mapema mno na tukimaliza uchunguzi au tukiwakamata
nitasema’’ alisema SACP Sanguti.
Alipotafutwa
kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, simu yake alipokea (Bodyguard)
wake na kusema kuwa kamanda huyo alikuwa msibani.
Mbali na
tukio hilo katika gereza la Songwe, pia taarifa zinasema kuwa katika gereza la
Ruanda hivi karibuni, alitoroka mahabusu mwenye asili yaEthiopia lakini tayari
amekamatwa.
0 comments:
Post a Comment