Friday, 24 January 2014

UJUMBE KUTOKA SEKTA BINAFSI WAKUTANA NA WIZARA YA NISHATI NA MADINI

1Mwenyekiti wa Taasisi ya sekta Binafsi (TPSF)   Bw. Reginald Mengi wa pili kushoto akieleza jambo wakati wa kikao baina ya TPSF na Wizara. Wanaosikiliza ni Mkurugenzi Mtendaji  wa TPSF Bw. Godfrey Simbeye na (katikati mbele) ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Bw. Eliakim Maswi. 2Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao baina ya Wizara ya Nishati na Madini na TPSF wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao hicho. 3Baadhi ya Wawakilishi kutoka Sekta Binafsi (TPSF) waliofika katika kikao hicho wakifuatilia kikao hicho.
………………………………………………………………………………
Asteria Muhozya,
Ujumbe kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), umekutana na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili masuala mbalimbali ya namna sekta binafsi zinavyoweza kushiriki katika uchumi wa gesi na mafuta nchini. 
Ujumbe huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw. Reginald Mengi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Bw.  Godfrey Simbeye pamoja na wawakilishi wengine wa Taasisi hiyo ulifika wizarani jana kukutana na uongozi wa Wizara.
Aidha, ujumbe huo ulipata nafasi ya kukutana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Bw. Eliakim Maswi na baadhi ya Watendaji wa Wizara wanaoshughulikia masuala ya Nishati, ambapo  TPSF walipata fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu namna ambavyo watashiriki katika uchumi  wa gesi.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wao,  wajumbe toka TPSF walieleza nia yao ya kushiriki katika uchumi wa gesi na kueleza  mikakati ya namna  watakavyoshiriki  ili sekta iweze kuwa na manufaa kwa  Watanzania wote na hivyo kuongeza  pato la nchi na  kufikia  maendeleo tarajiwa.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti wa sekta binafsi Bw. Reginald Mengi alitumia fursa hiyo kueleza kuwa, kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano ili  nchi iweze kuweza kufikia kule Watanzania na Taifa  linakotarajia kufika.
“Naondoka katika kikao hiki nikiwa na amani sana. Yaliyopita yamepita na yamekwisha. Tunataka kufanya kazi pamoja na Wizara katika sekta ya gesi. Tumekuja hapa kama Watanzania, tujue tutafanya kazi namna gani katika sekta hii”. Alisema Mengi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara hiyo Bw. Eliakim Maswi, aliushukuru ujumbe huo kwa kufika katika mazungumzo hayo na kueleza kuwa, nia ya Wizara na Serikali ni kuona Watanzania wote wanashiriki katika uchumi huo. Aidha, aliongeza kuwa, Wizara inayachukua mapendekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.
“Kwetu sisi tunataka kuona watanzania wanashiriki katika uchumi huu. Tuko tayari kufanya kazi na ninyi. Tufungue milango, tusaidiane huku tukiendeleza utulivu na uvumilivu. Mimi na wataalam wangu tutayafanyia kazi”. Alisema Maswi.

Related Posts:

0 comments: