Saturday, 4 January 2014

RAIA WA NIGERIA AKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA NCHINI TANZANIA

 
via HabariLeo — RAIA wa Nigeria, Okwubili Agu (40), amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) akiwa na pipi 71 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 54, alizokuwa amezimeza tumboni.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi majira ya saa 4 usiku katika uwanja huo. Nzowa alisema kuwa mtuhumiwa huyo 
alikamatwa na Kikosi Kazi kinachofanya kazi katika Uwanja huo, akiwa katika harakati za kusafiri na ndege ya KLM kwenda Amsterdam, Uholanzi.

Alisema kuwa askari hao walimshtukia na kuanza kumhoji, ambapo baada ya uchunguzi wao walimweka chini ya ulinzi na hadi sasa ametoa pipi 71 kwa njia ya haja kubwa.

Kamanda Nzowa alisema baada ya upekuzi, pia walimkuta Agu akiwa na hati ya kusafiria yenye namba AO3833671 iliyotolewa Juni 8, 2012 Lagos Nigeria.

Alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa kwa mahojiano zaidi huku akiendelea kuzitoa pipi hizo kwa njia ya haja kubwa.

0 comments: