Mama
Mzazi wa Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Mwanaidi Msengi,
amemsihi mwanawe kufanya kazi kwa bidii asimwangushe Rais Jakaya Kikwete
ili asije kujutia kumpa nafasi hiyo.
Mwanaidi alisema licha ya furaha kubwa
aliyonayo, anamuasa mtoto wake kuchapa kazi kwa bidii kama njia
mojawapo ya shukurani kwa Rais Kikwete kwa kumteua akiwa mwenyeji wa
kwanza kutoka Mkoa wa Singida kushika wadhifa huo nyeti
"Hii ni
heshima kubwa sana kwangu binafsi, ndugu zake, wakazi wa Kijiji cha
Kihunadi na Mkoa wa Singida, kwa hiyo lengo langu ni kumwombea mtoto
wangu Mangu asimwangushe Rais... Eee Baba (Mungu) msaidie mwanangu
atimize wajibu wake ipasavyo ili Rais Kikwete siku moja aseme hakukosea
kumpa Mangu ukuu wa polisi," alisema Mwanaidi.
Juzi
ndugu, jamaa na marafiki walifanya hafla ndogo iliyoambatana na vifijo,
nderemo na bashasha na wakazi wa Kijiji cha Kihunadi, Tarafa ya
Ilongero, mkoani Singida, alikozaliwa IGP huyo huku wakidai sasa kijiji
chao kitajulikana haraka ndani na nje ya Tanzania.
Walisema
licha ya kujulikana, changamoto mbalimbali zinazokikabili kijiji hicho
zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.
Mwanaidi
alisema Mangu alianza kumwonyesha mafanikio tangu Shule ya Msingi
Kinyagigi, kwani alikuwa na bidii ya kujisomea mara kwa mara alishika
nafasi ya kwanza au ya pili.
Kwa mujibu wa Mwanaidi, IGP Mangu ni mtoto wa pili kati ya saba aliowazaa.
"Mangu ni
wa pili kati ya watoto wangu saba baada ya kuolewa na baba yao, Jumbe
Omari Mangu aliyefariki Aprili 27, 1988. Jina la Jumbe linatokana na
kupewa kazi ya ujumbe wa wakoloni wakati wa ujana wake," alisema.
Wenyeji
wa kijiji hicho, walisema wamekuwa wakiamini Mangu atafika mbali kwa
kushika nafasi za juu za uongozi, kutokana na uadilifu, uchapaji kazi,
ukaribu wake na wananchi, uaminifu na uwazi.
Mwanaidi
alisema Mangu alipofaulu kwenda sekondari alilazimika kuomba ng'ombe kwa
mke mweza, ili akamuuze apate fedha za kugharimia masomo ya mtoto wake.
"Mke
mwenzangu alimtoa ng'ombe wake, lakini Mangu alipomuuza kwenye mnada
pale Singida mjini, aliibiwa fedha zote na alirudi nyumbani akilia
sana," alisema.
Alisema
baada ya hapo alimwambia mtoto wake kwamba, ataanza kutengeneza vyungu
kwa kutumia udongo wa mfinyanzi ili kupata fedha za kugharimia masomo
yake."Nashukuru Mangu alinielewa vizuri kwa sababu alishiriki kubeba
kichwani vyungu hivyo wakati wa kuviuza hadi kichwa chake kilikaribia
kuwa kipara. Nilibuni chanzo kingine cha mapato ambacho kilikuwa ni
kukoroga na kuuza pombe za kienyeji," alisema. Inadaiwa baba yake, IGP
Mangu alioa wanawake sita kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kupata
mtoto wa kiume. Wengi wa wake zake walikuwa wakizaa watoto wa
kike.CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment