MVUTO OLD TRAFFORD: MAN UNITED v SPURS, SAA 2.30 USIKU!
MWAKA
MPYA 2014 unaanza Januari Mosi England kwa Klabu zote 20 za Ligi
Kuu kushuka dimbani ikianza Mechi ya Swansea City na Manchester City na
kufuatia Mechi 8 zitakazoanza Saa 12 Jioni na Siku kufungwa kwa kimbembe
cha Old Trafford kati ya Mabingwa Manchester United na Tottenham.
Man United wako Nafasi ya 6, Pointi sawa
na Tottenham, wote wakiwa na Pointi 34 ikiwa ni Pointi 8 nyuma ya
Vinara Arsenal lakini ni Pointi 2 tu nyuma ya Timu ya 5 Liverpool ambao
nao wako Pointi 1 nyuma ya Everton walio Nafasi ya 4.
Wakati Timu zote, Man United na Spurs,
zikiwa zimeanza Msimu vibaya kwa Man United kufungwa Mechi 5 kati ya 15
za kwanza za Ligi na Tottenham kumtimua Meneja wao Andre Villas-Boas,
hivi karibuni Timu hizo zimeanza kufanya vizuri.
Man United wameshinda Mechi zao 6
zilizopita katika Mashindano yote wakati Tottenham, chini ya Meneja mpya
Tim Sherwood, ambae hutumia Mfumo wa 4-4-2, hawajafungwa Mechi ya Ligi
tangu atwae himaya Wiki mbili zilizopita.
Kwenye Mechi hii, Man United
wanatarajiwa kuwa nae Wayne Rooney ambae aliikosa Mechi Jumamosi
waliyowafunga Norwich City Bao 1-0 baada kupona maumivu ya Nyonga lakini
huenda wakamkosa Robin van Persie, ambae, licha ya kupona majeruhi yake
na kuanza Mazoezi, huenda akawa si fiti kwa Mechi baada kuwa nje Mwezi
mzima.
Katika Mechi ya kwanza ya Ligi Msimu huu
iliyochezwa White Hart Lane, Spurs na Man United zilitoka 2-2 lakini
mara ya mwisho kukutana Old Trafford, Tottenham walishinda Bao 3-2 hapo
Septemba 2012 hiyo ikiwa ni mara yao ya kwanza kushinda Uwanjani hapo
tangu Mwaka 1989.
Nao Liverpool, ambao Siku ya Krismasi
walikuwa kileleni na baada kuchapwa mfululizo na Man City na Chelsea,
sasa wako Nafasi ya 5, wataikaribisha Hul City Uwanjani Anfield na
huenda hii ndio Mechi yao ya kufuta machungu yao ya kuchapwa Mechi mbili
mfululizo.
Lakini katika Mechi yao ya kwanza ya Ligi kati yao, Mwezi mmoja uliopita, Hull City iliitandika Liverpool Bao 3-1.
Everton walitumia kipigo cha Liverpool
toka kwa Chelsea na kutua Nafasi ya 4 baada ya kushinda Uwanjani kwao
Goodison Park walipoipiga Southampton 2-1 na safari hii wanasafiri
kwenda kucheza na Stoke City ambayo imefungwa mara moja tu Nyumbani kwao
Msimu huu.
Arsenal, ambao wamemaliza Mwaka 2013 kwa
kuwa kileleni mwa Ligi baada kuitungua Newcastle Bao 1-0 huko St James
Park, Jumatano watakuwa Nyumbani Emirates kuivaa Cardiff City ambao
hawana Meneja baada kumtimua Malky Mackay hivi Juzi.
Lakini, ingawa Arsenal wako kileleni, nyuma yao kwa Pointi 1 wapo Man City na Chelsea wako Pointi 1 nyuma ya City.
Chelsea, ambao Jumapili waliitwanga Liverpool 2-1 Uwanjani Stamford Bridge, watakuwa Ugenini kucheza na Southampton.
Man City wanaweza, kwa muda, kukwaa
kilele cha Ligi Siku hii ya Mwaka mpya kwani Mechi yao ya Ugenini na
Swansea City ndio ya kwanza kabisa kwa Mwaka 2014.
RATIBA MECHI ZIJAZO:
[Saa za Bongo]
Jumatano Januari 1
1800 Arsenal v Cardiff
1800 Crystal Palace v Norwich
1800 Fulham v West Ham
1800 Liverpool v Hull
1800 Southampton v Chelsea
1800 Stoke v Everton
1800 Sunderland v Aston Villa
1800 West Brom v Newcastle
2030 Man United v Tottenham
0 comments:
Post a Comment