Saturday, 25 January 2014

KAULI YA CCM BUKOBA MJINI KUHUSU RIPOTI YA CAG

3Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye  picha na makita
 TAMKO LA CHAMA CHA MAPINDUZI WILAYA BUKOBA MJINI TAREHE 24/01/2014 KWA  VYOMBO VYA HABARI 

Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukoba Mjini kupitia kikao chake cha kawaida cha Kamati ya Siasa ya H/Kuu ya Wilaya iliyoketi leo tarehe 24/01/2014.

Kimepokea na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Ukaguzi maalum uliofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba katika kipindi cha miaka 3 ya 2010/2011, 2011/2012 na 2012/2013.

Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukoba Mjni kinaunga mkono taarifa hiyo ya CAG. Aidha kinaipongeza na kuishukuru 
Kamati Kuu ya CCM chini ya M/Kiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuupokea mgogoro uliokuwepo baina ya Madiwani wa Manispaa ya Bukoba na kuushughulikia na kuhakikisha unafika mwisho.

Vile vile tunaipongeza na kuishukuru Timu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa umakini na kuyabainisha mapungufu yaliyopo kwenye taarifa hiyo ya Ukaguzi.

Chama Wilaya kinaihimiza Serikali kusimamia na kuhakikisha hatua za Kisheria na Kinidhamu zinachukuliwa haraka dhidi ya wale wote waliohusika na ubadhilifu huo.

Pia Chama kinawaagiza Madiwani kuendelea na vikao vyao vya Kisheria ili kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM unakamilika kama ilivyopangwa.

Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukoba Mjini kinaendelea kuwashukuru Wananchi wa Bukoba Mjini kwa utulivu wao waliouonyesha katika kipindi chote cha mgogoro.

Tunaomba waendelee kushirikiana na Chama na Serikali yake katika kuleta Maendeleo ya Bukoba Mjini.

"UMOJA NI NGUVU NA UMOJA NI USHINDI"
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI 

 

Related Posts:

0 comments: