Saturday, 4 January 2014

ASKARI WA JWTZ MBARONI KWA KUTUHUMIWA KUUA WATU WAWILI


Dar es Salaam. Polisi Mkoa wa Ilala inamshikilia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), mwenye cheo cha meja wa Kikosi Miguu Kibaha kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwapiga risasi vijana wawili wakazi wa eneo la Pugu Kinyamwezi, wakati wa shamrashamra za mkesha wa mwaka mpya.
Vijana waliopoteza maisha katika sakata hilo ni Ibrahim Mohamed (16) na Abubakar Hassan (14).

Waliojeruhiwa na hali zao zinaendelea vizuri kwenye Hospitali ya Amana ni Lugano Wanga na Khamis Abuli, wakazi wa Pugu na wote wana umri wa miaka 16.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mwanajeshi huyo inadaiwa siku ya tukio akiwa eneo hilo la Pugu Kinyamwezi, gari lake lilizingirwa na vijana waliokuwa wakishangilia mwaka mpya na baadhi yao walipanda juu ya gari hilo ndipo milio ya risasi iliposikika.
Pia, kundi hilo la vijana linadaiwa kuvunja vioo vya baadhi ya magari yaliyokuwa yanatumia barabara hiyo.
Wakati huohuo, washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokamilika.
Wakili wa Serikali, Yasinta Peter alimweleza Hakimu Mkazi, Geni Dudu kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Dudu aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 14 na kuamuru washtakiwa hao kuendelea kukaa rumande kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Chibago Magozi (32) mfanyabiashara na mkazi wa Vingunguti Machinjioni, John Mayunga (56) mfanyabiashara na mkazi wa Kiwalani na Juma Kangungu (29) mkazi wa Vingunguti.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi, Longishu Losingo (29) na Masunga Makenza (40) dereva na mkazi wa Kitunda, Paulo Mdonondo (30) mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa (40) Mkazi wa Vingunguti, Zacharia Msese (33) mkazi wa Buguruni, Msungwa Matonya (30) mkazi wa Vingunguti na Ahmad Kitabu (30) mkazi wa Mwananyamala wilayani Kinondoni.

 Na Waandishi Wetu, Mwananchi
 

Related Posts:

0 comments: