Thursday, 9 January 2014

ABIRIA WA TRENI WAKWAMA SIKU SABA WAANDAMANA MPAKA KWA MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dr. Rehema Nchimbi

Abiria waliokuwa wakisafiri kwa reli ya kati kutoka Kigoma kwenda Morogoro na Dar es Salaam, jana waliandamana hadi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakipinga kusitishwa kwa safari yao.

Abiria hao zaidi ya 200, walichukua hatua hiyo kwa lengo la kupinga kitendo cha uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuahirisha safari yao kutokana na kuharibika kwa njia ya reli eneo la Gulwe na Godegode wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.


Zaidi ya abiria 1,600 ambao walianza safari yao tangu Januari 2, mwaka huu, walifika jana asubuhi katika Stesheni ya Dodoma, lakini walishindwa kuendelea na safari yao kutokana na kuharibika kwa kipande hicho cha reli ambacho kilisombwa na mafuriko.


Mmoja wa abiria hao, Alphonce Evarist, alisema tangu walipoanza safari yao imekuwa na matatizo na kwamba wamekaa njiani kwa siku nane. Evarist alisema wakiwa Kigoma, waliambiwa hawawezi kusafiri kwa kuwa reli ilikuwa imezolewa na mafuriko Dodoma na walipofika walielezwa tena hawawezi kusafiri kwa kuwa reli imeharibika.


“Ni reli gani hiyo ambayo inatengenezwa kwa muda wa siku saba. Tangu tunatoka Kigoma tunaambiwa reli imeharibika, tunafika hapa tunaambiwa hatuwezi kusafiri kwa kuwa reli imeharibika. Kwa nini mnatudanganya kama watoto wadogo?'” Alihoji.


“Tuna watoto na mizigo ya kuharibika njiani. Tumeuza kila kitu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wetu wasife njiani, lakini tena tumefika hapa tunaambiwa kuwa hakuna safari. Kwa kweli mnatukatisha tamaa na huu usafiri,” alisema na kuongeza:

“Tumeishiwa kila kitu na hatujui hatma ya safari hii, tunachokuomba Mkuu wa Mkoa ututafutie usafiri wa kutufikisha tunapokwenda kwa sababu tumeshamaliza fedha zote njiani na hatujui tutaondoka lini,” alisema.

Naye Mwajuma Hassan, aliiomba serikali kushughulikia tatizo la usafiri wa reli. “Tumeona serikali yetu ikishughulikia suala la Tokomeza Ujangili kwa haraka na baadhi ya hatua zikichukuliwa, iweje suala la reli lishindikane?'” Alihoji.


Kwa upande wake, Hashim Mohamed, alisema kitendo hicho cha ofisi ya Mkuu wa Mkoa kimeonyesha ni jinsi gani serikali inavyowajali Watanzania bila kujali itikadi ya vyama vya siasa, dini na rangi.


Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, aliwasihi abiria hao kuwa wavumilivu.


“Ni kweli kwa kipindi hichi reli katika eneo la Gulwe na Godegode, ilikuwa imeharibika kutokana na mafuriko na ilishatengenezwa, lakini kipande hicho ni korofi na mara nyingi huwa kinakumbwa na mafuriko, kwa hiyo baada ya kutengeneza yalitokea mafuriko tena na kuisomba reli hiyo,” alisema.


Pia, aliiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Dodoma Mjini na uongozi wa TRL, kuhakikisha usalama wa abiria hao kwa kipindi chote watakapokuwa mkoani hapa hadi usafiri utakapopatikana.


Aidha, aliuagiza uongozi wa TRL kuhakikisha abiria wote wanapata huduma zote muhimu bure ikiwamo ya chakula hadi hapo watakapoanza safari kurejea makwao.

Alisema kwa wakati huo hapakuwapo na usafiri wa magari kuwafikisha wanakokwenda kutokana na magari yote kuondoka, hivyo aliwataka wavumilie hadi muda waliopewa na TRL.

Mhandisi mitambo wa TRL mkoani Dodoma, John Mandalu, aliwaomba abiria wote waliokuwapo stesheni, kuingia kwenye mabehewa yao ili kuhesabiwa na kupatiwa msaada wa chakula hadi hapo safari yao itakapokamilika.


Mkuu wa Kituo cha Reli mjini Dodoma, Zakaria Kilombero, aliliambia NIPASHE kuwa wanatarajia kuwasafirisha abiria waliokwama kuanzia juzi saa 11:00 jioni kama watakuwa wamekamilisha ukarabati unaoendelea kwenye maeneo ya Gulwe na Godegode.


Kuhusu kuwapa abiria chakula, alisema anasubiri maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TRL ili zoezi la kuwapa fedha abiria lianze.


“Kila abiria atapewa Sh. 3,500 kwa maana ya chai Sh. 1,500 na chakula Sh. 2,000, fedha hizo ni kwa siku moja tu,” alisema.


TRL YASOGEZA TENA USAFIRI

Jijini Dar es Salaam, jana TRL ilitoa taarifa ikisema kwamba usafiri wa treni ya abiria iliyopangwa kuondoka jana saa 3:00 usiku kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, Mpanda na Kigoma, umeahirishwa kutokana na mafuriko yaliyotokea katika stesheni ya Gulwe na Godegode mkoani Dodoma.

Badala yake, taarifa hiyo ilieleza kuwa treni hiyo imepangwa kuondoka Dar es Salaam leo saa 11:00 jioni na treni ya kawaida ya Ijumaa itaondoka saa 3:00 usiku ikisema ni kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa kampuni.


Meneja Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.


Alisema Kampuni huchukua tahadhari za haraka wakati tukio kama hilo linapojitokeza kwa kutoa taarifa mapema kwa abiria ambao wamo ndani ya treni hiyo iliyopata tatizo na kwamba gharama zote huchukuliwa na kampuni ikiwamo ya chakula.


“Ni wajibu wa TRL kuwahudumia abiria waliopo ndani ya treni tu ikiwa tatizo limetokea, lakini taarifa ikitolewa mapema na abiria hajapanda treni, hatuhusiki kwa lolote,” alisema.


Maez alitolea mfano wa abiria waliokwama katika stesheni ya Gulwe ambayo mafuriko yametokea kuwa madai yao yatashughulikiwa na TRL kwa mujibu na tiketi zao.

Aidha, menejimenti ya TRL, imewaomba radhi wadau wote wanaotumia usafiri wa treni kutokana na usumbufu wote uliojitokeza.

Imeandikwa na Jacqueline Massano, na Peter Mkwavila, Dodoma, Leonce Zimbandu, Dar. 
SOURCE: NIPASHE
10th January 2014

Related Posts:

0 comments: