Saturday, 2 August 2014

KIONGOZI TFF ASHUHUDIA YANGA SC ‘INAVYOLALIWA’ MSUMBIJI, ASEMA...


 
MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau leo ameshuhudia namna klabu ya Yanga SC inavyohujumiwa nchini Msumbiji.
Asubuhi ya leo, Kidau ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TFF akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maputo, nchini hapa alikutana kijana mmoja akiwa amevalia jezi Yanga ambayo amenunua kwa watu wanaouza bila idhini ya klabu hiyo.
Kidau alifika Uwanja wa Ndege kuwapokea washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC waliokuja kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi ya wenyeji, Msumbiji kesho.
Kidau kushoto akiwa na raia wa Msumbiji aliyenunua jezi ya Yanga SC mjini Beira

Kijana huyo raia wa Msumbiji, Magnum alisema kwamba jezi hiyo aliinunua Beira na anafahamu kwamba Yanga SC ni timu ya Tanzania, lakini haijui.
“Nimependa jezi nzuri, rangi nzuri nikanunua,”alisema kijana huyo ambaye alifika uwanja wa ndege kupata huduma za kibenki.
Alisema amenunua jezi hiyo kwa thamani ambayo ni sawa na fedha za Tanzania Sh. 15,000 na kwamba watu wengine pia wananunua kwa wingi na kuvaa jezi hizo nchini Msumbiji.
Kidau alisema kwamba Yanga SC na watani wao Simba SC wanapoteza fedha nyingi kutokana na kupuuza bishara ya jezi na bidhaa nyingine zenye nembo zao.
“Sasa watu ambao wanajua kama hii ni bishara nzuri, ndiyo wanajipatia fedha nyingi kirahisi namna hii, hii ni biashara kubwa sana, klabu nyingi Ulaya zinanufaika mno kwa biashara hii,”alisema kiungo wa zamani wa Milambo ya Tabora, Simba SC na timu ya Taifa, Taifa Stars.
Pamoja na ukweli huo kwamba jezi za timu ni biashara inayoziingizia fedha nyingi hata klabu kubwa Ulaya, lakini bado viongozi wa Yanga SC  hawajaonyesha kutaka kutumia fursa hiyo kuinufaisha klabu yao kiuchumi.
Jezi za Yanga pamoja na mahasimu wao, Simba SC zinapatikana karibu Afrika Mashariki yote na nchi nyingine jirani ikiwemo Msumbiji.
Wapembuzi yakinifu wa masuala ya biashara hiyo wanaamini, kwa mwaka Simba na Yanga zinakosa si chini ya Sh. Milioni 500 kila klabu kwa kupuuza biashara ya jezi pekee.

0 comments: