Sunday, 9 February 2014

MUUZA MAGAZETI AJITOKEZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA KALENGA KUPITIA CHADEMA


Aidan Pugili
WAKALA wa magazeti mjini Iringa, Aidan Pugili (34) amejitokeza kuwania ubunge katika jimbo la Kalenga mkoani Iringa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Uchaguzi mdogo wa kujaza kiti hicho kilichoachwa wazi na Dk William Mgimwa aliyefariki Januari 1, mwaka huu, utafanyika Machi 16, mwaka huu.

Akitumia umaarufu wake wa kuuza magazeti mjini hapa, Pugili aliyesindikizwa na baadhi ya wauza magazeti wenzake alichukua fomu za Chadema kwa staili ya aina yake huku akisindikizwa na magari madogo manne ya kukodi.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kuchukua fomu hizo anazotarajia kuzirudisha Jumanne, alisema amejipima na ameona anatosha kuiwakilisha Chadema katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka katika chama hicho kura za maoni kwa wagombea watakaojitokeza zitapigwa Jumatano ya Februari 12.

Pugili ambaye pia ni mjasiriamali aliyewekeza biashara ndogondogo mjini Iringa na Mbeya alisema tangu Chifu Mkwawa afariki dunia kwa kujiua mwenyewe wananchi wa Kalenga iliyokuwa ngome kuu ya chifu huyo hawajawahi kupata mwakilishi mwenye nguvu.
“Nina uwezo wa kuwa mwakilishi wao. Ni mzoefu katika siasa za upinzani na nimekuwepo ndani ya Chadema kwa muda mrefu,” alisema.

Alisema ajenda yake ya kwanza endapo atapewa ridhaa ya chama chake na wananchi wa jimbo la Kalenga itakuwa ni kupambana na ufisadi ndani ya halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Ajenda yake ya pili alisema itakuwa ni kuleta mapinduzi katika kilimo kwa kuwashawishi wagiriki wenye mashamba makubwa ya tumbaku katika jimbo hilo kugawa ardhi wasiyoitumia kwa wananchi.

“Lakini ili kilimo kiwe na tija Chadema tunataka kuondokana na biashara ya kuwatumia mawakala kusambaza pembejeo,” alisema.

Alisema watapigania uanzishwaji wa Mamlaka ya Kilimo Tanzania itakayosimamiwa na serikali ili kuratibu kwa uhakika ukopaji na usambazaji wa pembejeo.

“Nataka wananchi wa jimbo la Kalenga ambao asilimia 80 ni wakulima wanufaike na kilimo ili waweze kupeleka watoto wao shule,” alisema.

Alisema afya na utalii zitakuwa ajenda zake zingine muhimu katika kinyang’anyiro hicho.

“Afya ni majisafi, matibabu na lishebor, nitapiga kuhakikisha wananchi wa Kalenga wanapata huduma hizo muhimu,” alisema.

Alisema  serikali ya CCM imeyatelekeza makumbusho ya Mkwawa yaliyopo Kalenga na kufanya jimbo hilo na watu wake wakose mapato mengi kutoka kwa watalii.

“Nitahamasisha utalii wa makumbusho hayo. Nataka dunia isisahau historia ya chifu Mkwawa na katika hilo nitakuwa naenzi ushujaa wake,” alisema.

Related Posts:

0 comments: