Saturday, 1 February 2014

MERSON ASEMA NA KUDAI KUWA CHELSEA ITAIFUNGA MAN CITY

 

RTO1 c5d0e
NI wababe. Wanatembeza vichapo vinene kila wanapocheza na timu kubwa. Matokeo huwa ni 6-3, 5-1, 4-1. Hawa ni Manchester City. Jumatatu usiku watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani Etihad kukipiga na wababe wenzao, Chelsea. 
Lakini 'mwendawazimu' mmoja ametabiri kwamba katika pambano hilo, Chelsea itaibuka mbabe mbele ya Manchester City, tena katika uwanja wa ugenini na kila shabiki atashangaa.
Kiungo wa zamani wa Arsenal, Paul Merson amedai kwamba ana kila sababu ya kuamini kuwa Chelsea itaichapa Manchester City katika pambano hilo la Jumatatu usiku na kukomesha ubabe wao unaozidi kushika kasi katika miezi ya karibuni.
"Ukweli ni kwamba Chelsea hawatakwenda Etihad kwa ajili ya kujihami. Manchester City hawatakuwa na Sergio Aguero na wanapomkosa wanakuwa timu tofauti kabisa. Wawili waliopo mbele, Edin Dzeko na Alvaro Negredo watapambana vilivyo na John Terry na Gary Cahill. Wale hawawezi kushuka chini na kusumbua kama Aguero anavyofanya," alisema Merson.
"Kama wakicheza kama ninavyofikiri, sioni jinsi gani Chelsea itapoteza mechi hii. Kama wakienda kwa ajili ya kujilinda Man City watatengeneza nafasi nyingi. Lakini mara kadhaa nimeiona Man City wakiwa wazembe katika ulinzi," aliongeza Merson.
"Crystal Palace, Cardiff na hata
Watford wamekwenda pale na kutengeneza nafasi na wangeweza kushinda mechi. Katika mechi kubwa huwa wanapambana zaidi na itavutia kuona nini kitatokea wakati watakapocheza na moja kati ya timu kubwa Ligi Kuu England kwa sasa kama Chelsea ambayo ina mastaa wa kuweza kuwashtukiza."

Katika hali ya kushangaza, Merson ametabiri kwamba pambano la leo Jumamosi kati ya Stoke City na Manchester United litaisha kwa sare licha ya Man United kupata nguvu kwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Juan Mata.
"Bado kuna kazi kubwa ya kufanya Manchester United. Wana Robin van Persie, Wayne Rooney na Juan Mata katika timu yao kwa sasa, lakini sehemu ya ulinzi haijabadilika na hata kiungo kipo hivyo hivyo kwa hiyo nadhani Stoke haitapoteza mechi hii," aliongeza Merson huku akizitabiria ushindi Arsenal na Liverpool ambazo zinacheza na Crystal Palace na West Brom. Chanzo: mwanaspoti

0 comments: