Wednesday 16 April 2014

SIMBA YAJIFICHA ZANZIBAR KUTAFUTA SUMU YA KUWAUA YANGA JUMAMOSI



_DSC0696
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba sc wamesahau vipigo vyote vya mechi za nyuma na sasa wameelekea visiwani Zanzibar kuweka kambi kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga SC aprili 19 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Katibu mkuu wa Simba sc, Ezekiel Kamwaga ameuambia mtandao huu dakika chache zilizopita kuwa kikosi cha wachezaji 18 kimeondoka jioni hii kwenda Zanzibar kutafuta sumu ya kuwaua Yanga.
“Timu ipo katika hali nzuri. Yaliyopita si ndwele, sasa akili yetu ni mchezo wa jumamosi dhidi ya mtani. Tuna matarajio makubwa ya kushinda mechi hiyo”. Amesema Kamwaga.
Kamwaga amewatoa hofu mashabiki wa Simba ambapo amewahakikishia kuwa maandalizi wanayoenda kuyafanya ni ya hali ya juu.
“Tumefanya vibaya msimu huu kinyume na matarajio ya mashabiki wetu”.
“ Kuwafunga Yanga mechi ya mwisho itakuwa faraja kubwa kwao. Uongozi umejiandaa vizuri na timu ipo katika hali nzuri kabisa”. Ameongeza Kamwaga.
Hata hivyo taarifa zilizoenea mchana wa leo ni kuwa wachezaji wa Simba waligoma kwenda Zanzibar wakishinikiza kulipwa mishahara yao ya mwezi huu.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe alilazimika kuwalipa fedha wachezaji wote na benchi la ufundi ili kuokoa jahazi, na jioni hii safari ilianza.
Simba sc wataingia uwanjani wakiwa na malengo ya kushinda na kulinda heshima yao.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Dravko Logarusic alikaririwa na mtandao huu akisema mechi ya mwisho ameipa uzito wa hali ya juu, hivyo alihitaji kambi kuwepo maeneo tulivu.
Mechi hiyo haitakuwa na presha kubwa kwani matokeo kwa timu zote hayatabadili chochote kwa maana ya Simba kupanda nafasi za juu wala Yanga kuchukua ubingwa.
Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 55 baada ya kucheza mechi 25, pointi nne nyuma ya Azam fc waliopo kileleni kwa pointi 59, huku tayari wakiwa wameshajitangazia ubingwa kwasababu hakuna klabu inayoweza kuzifikia pointi hizo.
Wachezaji waliondoka jioni hii ni walinda mlango Ivo Philip Mapunda na Yaw Berko.
Walinzi ni William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ Joseph Owino, Donald Mosoti, Nassor Masoud ‘Chollo’.
Viungo Henry Joseph, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Uhuru Suleiman Jonas Mkude, Said Ndemla, Awadh Juma, Ramadhani Singano ‘Mesi’, Haroun Chanongo, Amri Kiemba na washambuliaji ni Amisi Tambwe na Zahor Pazi.

0 comments: