Saturday 19 April 2014

MECHI YA 77 SIMBA NA YANGA LIGI KUU TANGU 1965

Yanga_65a60.jpg
Picha kwa hisani ya sw-ke.facebook.com
Na Daniel Mbega
"KITIMTIMU, mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu kaingiaje!" Naam, hilo ni chagizo la wimbo maarufu wa mashabiki wa Yanga kila wanapoishangilia timu yao, hasa inapocheza na Simba.
Lakini chagizo hilo litakumbana na kibwagizo cha mashabiki wa Simba, maarufu kama Mchacho Group (ambao sasa wameongezewa sapoti na tawi la Mpira Fedha) watakaokuwa wakiimba "Amesimama kidedea, eeee kidedea!"
Timu hizo mbili zinapopambana katika mechi ya Jumamosi hii Aprili 19, kukunja jamvi la Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa msimu wa 2013/2014, kila mtu anatazama nini kitatokea, iwe uwanjani ama nje ya uwanja.
Mechi baina ya timu hizi mbili kongwe katiba katika historia ya kandanda nchini huwa zinatawaliwa na vituko vingi mno. Kuvunja nazi, kuoga maji ya maiti, kuruka ukuta, kuingia uwanjani kinyumenyume na mengine kama hayo hutajwa kwamba ni sehemu ya kuhanikiza ushindani.
Hata hivyo, kwa sasa hawawezi kuruka ukuta kama ilivyokuwa miaka ile ya zamani, wala hawawezi kuoga maji ya kuoshea maiti au kuvunja nazi hadharani, kwa sababu Sheria za Soka haziruhusu ushirikina na tayari timu hizo mbili zimekwishawahi kutozwa faini kwa vitendo hivyo.
Simba ikiwa inatokea Zanzibar, na Yanga ambayo ilikuwa Kawe jijini Dar es Salaam, zinapambana Jumamosi hii zikitaka kulinda heshima tu, kwa sababu ubingwa tayari umekwishachukuliwa na Azam FC iliyofikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.
Ushindi wa Azam wa mabao 2-1 nyumbani kwa Mbeya City Jumapili iliyopita uliifanya iweke rekodi mpya kwa kuwa timu ya nane katika historia ya soka nchini kunyakua ubingwa huo ambao umekuwa ukitwaliwa na Simba na Yanga pekee. Mara ya mwisho kwa timu nyingine kutwaa ubingwa (mbali ya Simba na Yanga) ilikuwa mwaka 2000 wakati Mtibwa Sugar ilipotwaa kwa mara ya pili mfululizo ubingwa huo wa Bara.
Lakini pia ushindi wa Azam ulivunja rekodi ya kutofungwa ya Mbeya City kwenye uwanja wake wa nyumbani katika msimu huu, huku Azam ikiendelea kushikilia rekodi yake nyingine ya kutopoteza hata mechi moja katika msimu huu. Sijui leo hii hali itakuwaje.
Yanga yenyewe imeshika nafasi ya pili kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya JKT Oljoro na sasa inahitaji vitu viwili tu – kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 msimu wa 2011/2012 pamoja na kulinda hadhi yake, huku Simba ikitaka kuendeleza ubabe kwa vijana hao wa Jangwani kwa kuwa hakuna itakachopoteza katika nafasi yake ya nne iliyoifikia.
Lakini kwa upande mwingine ushindi ni muhimu sana kwa Simba ikiwa inataka kulinda hadhi yake japo kwa kumaliza ikiwa ya nne, kwa sababu ikiwa itapoteza mchezo huo, basi inaweza kujikuta ikimaliza ikiwa ya sita msimu huu. Hii ni kwa sababu mpaka sasa ina pointi 37 wakati nyuma yake kuna timu mbili za Kagera Sugar na Ruvu Shooting ambazo zina pointi 35 kila moja.
Kagera Sugar inayoshika nafsi ya tano ikishinda ugenini kwa Coastal Union na Ruvu Shooting ikiwalazama maafande wa Rhino Rangers ambao tayari wamekwishashuka daraja, zinaweza kuipiku Simba kimzaha mzaha tu.
Kelele za: "Simba! Simba! Simba!" na zile za: "CCM! CCM! CCM!" zitasikika kwenye Uwanja wa Taifa, lakini zitahitaji kuangalia matokeo ya uwanjani yakoje, vinginevyo upande mmoja unaweza kuzizima.
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Mandhari haya ndiyo yaliyokuwepo Jumapili Oktoba 20, 2013 kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, wakati Simba na Yanga zilipoumana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014.
Wakati Yanga, ambayo ilikuwa inatetea ubingwa wake huku ilikiwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo, ilikuwa inatafuta ushindi ili kukwea kileleni lakini pia kulipa kisasi cha mabao 5-0 ilichokipata mwaka 2012 katika mchezo wa mwisho. Jambo hili lilionekana kuwa ni ndoto baada ya kushindwa kuyalinda mabao yake matatu iliyoyapata katika kipindi cha kwanza, hivyo kuifanya Simba isawazishe na kuleta matokeo ya ajabu ya sare ya 3-3.
Simba wao walikuwa na mambo mawili: Kwanza, walitaka kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Mei 17, 2013, lakini pili, walikuwa wanatafuta ushindi ili kujiweka sawa zaidi na kutwaa ubingwa baada ya kukosa hata nafasi ya pili.
Kama wachezaji wa timu hizo watatulia na kutandaza soka, huku wakiacha ubabe na kufuatisha kelele za mashabiki jukwaani, hakika hii itakuwa burudani safi ya kufungia msimu.
Mechi zao
Hii itakuwa mechi ya 77 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekeza mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu gani.
Hata hivyo, katika mechi 76 zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 29, wakati Simba imeshinda mara 22. Timu hizo zimetoka sare mara 25 huku mabao 162 yakifungwa. Kati ya mabao hayo, Yanga imefunga 86 na Simba imefunga 75. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi ya Muungano.
MECHI YA 77 SIMBA NA YANGA LIGI KUU TANGU 1965

0 comments: