Saturday 19 April 2014

SITTA AHAHA KULINUSURU BUNGE MAALUMU LA KATIBA


Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta anahaha kulinusuru Bunge hilo, baada ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zilisema Sitta anawasaka viongozi wa Ukawa kwa lengo la kukaa nao katika meza ya mazungumzo, kutafuta maridhiano yatakayowezesha kundi hilo kurejea bungeni.
Sitta jana aliliambia Mwananchi kuwa wako njiapanda, kwa sababu hawafahamu kama wajumbe hao wa Ukawa wametoka tu nje ya ukumbi na watarudi au wamejiuzulu.  

"Hapa ninapozungumza na wewe nimesitisha kwenda mapumziko ya Pasaka... Nimewapigia simu Lipumba (Ibrahim) na Mbowe (Freeman), lakini hawapokei simu," alisema Sitta na kuongeza;
"Niliyempata ni Mbatia (James) peke yake na ameniambia yeye yuko na wenzake na hana uamuzi wa pamoja...Nataka nikutane nao ana kwa ana nasubiri kama inawezekana tufanye mazungumzo."
Aliongeza: "Nasubiri hata kama watatuma mwakilishi wao tukae tuzungumze hili jambo, lakini mpaka sasa sijaona mwakilishi yoyote...huwezi kuamini sijaenda Pasaka niko hapa Dodoma."
Sitta alisema pamoja na viongozi hao wawili wakuu wa Ukawa hawapokei simu, lakini amefanya jitihada ikiwamo kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), lakini hadi jana mchana alikuwa hajajibiwa.
"Sitaki kuongeza chochote kuhusu hili jambo kwa sababu kwa mazingira yenyewe nikisema chochote ninaweza kuharibu japo nina maoni yangu binafsi kuhusu hili, lakini sitaki kusema sasa," alisema Sitta.
Jana gazeti hili lilimtafuta Mbatia ambaye alikiri kuzungumza na Sitta. "Ni kweli amenipigia simu na nimemwambia kwamba nimemsikia, lakini siwezi kufanya uamuzi peke yangu, lazima nishuriane na wenzangu."
Hata hivyo, Mbatia alisema kwa mtizamo wake hadhani kama Sitta anaweza kutatua mvutano uliopo na kwamba wanaopaswa kusimamia suala hilo ni viongozi wa vyama vya siasa vinavyovutana.
"Mimi naamini katika maridhiano, lakini vyama vya siasa ndivyo vinaweza kutatua mzozo huu, kwa hiyo viongozi wa CCM ndiyo wanaweza kuonyesha nia ya kuzungumza, Sitta ni kiongozi wa Bunge ambaye kazi yake ni kusimamia uendeshaji wa vikao, hivyo suala la maridhiano kwake ni kumtwisha mzigo mzito ambao hapaswi kuubeba," alisema Mbatia.
Kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo za 2014, zinasema kuwa ili ibara au Rasimu ya Katiba iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kwa pande zote za Muungano.Soma zaidi>>>>>

0 comments: