Monday 28 April 2014

! KUACHA KAZI MAN U, MOYES KALAMBA SH BILIONI 17.5 NA SASA ANAKULA BATA





DAVID Moyes amepoteza kazi, hakuwa na ujanja na ilikuwa lazima iwe hivyo kwa kuwa asingeweza kubadilisha mambo.
Ndani ya miezi kumi, tayari Man United ilikuwa imepoteza mechi 11 za Ligi ya Mabingwa Ulaya, hali iliyolazimisha kukatisha mkataba wake huo wa miaka sita.

Hapa nyumbani imekuwa ni kawaida kabisa kuwaona Yanga na Simba wakiingia kwenye mgogoro mkubwa na makocha wa kigeni na wazalendo kuhusiana na malipo yao.
Wanapokatisha mkataba, kumlipa kocha inakuwa ni kazi ngumu na hadi kufikia mgogoro mkubwa. Kama unakumbuka wakati ule Milovan Cirkovic alilazimika kuokolewa na Rahma Al Kharoos ‘Malkia wa Nyuki’ kwa kuwa Simba ilishindwa kumlipa Sh milioni 36 zilizokuwa zinatakiwa kwa ajili ya kuvunja mkataba wake.

Lakini mkataba wa miaka sita umevunjwa kwa kitita cha pauni milioni 7 (zaidi ya Sh bilioni 17.5), fedha ambazo zinaweza kuifanya Yanga, Simba au timu nyingine ya Tanzania kuwa tajiri zaidi kama ikizikamata.

Moyes amelipwa fedha hizo ambazo zinajumuisha mshahara wake wa mwezi, fedha ya kuvunja mkataba pamoja na malipo ya usumbufu kutokana na uvunjani huo wa mkataba.

Lakini wakati wa uvunjani mkataba wake, kuna mambo kadhaa ya kiufundi yalifanyika ambayo yanaashiria namna gani walioendelea katika michezo, mikataba yao inavyokuwa na utaalamu.


Katika mkataba wa Moyes, ilikuwa hivi. Kama angeifikisha timu katika nne bora na kuweza kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi wakimfukuza ilikuwa ni lazima alipwe kitita cha pauni milioni 9 (zaidi ya Sh bilioni 22.5).
Pamoja na maji kuwafika shingoni, uongozi wa Man United uliendelea kufanya subira katika jambo moja. Kuwa iwapo watafungwa mechi itakayothibitisha kuwa hawatakuwa katika nne, maana yake wamekosa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, hapo watatoa pauni milioni 7 badala ya milioni 9.
Mkutano wa mwisho waliofanya wamiliki wa Man United, Joe Glazer na wenzake ilikuwa ni kujaribu kuokoa pauni hizo milioni 2 wakati Moyes anaondoka.
Mechi dhidi ya Everton ndiyo ilikuwa na majibu, kama Man United wangepoteza maana yake uhakika wasingefika nne bora na malengo ya uongozi kuokoa pauni milioni 2 ungekuwa umetimia.
 
Baada ya Man United kufungwa mabao 2-0, viongozi wa Man United waliandaa mkutano mara moja kumtaarifu kocha huyo kuhusiana na suala hilo na taarifa zikaanza kuvuja.

Huenda wengi walishangazwa na namna ungozi wa Man United ulivyochelewa kumuondoa. Lakini mambo mawili yalikuwa ya msingi zaidi kwao kuliko matakwa ya mashabiki.
Kwanza kuangalia kama kungekuwa na mabadiliko ili Moyes aendelee, lakini kuhakikisha kama imeshindikana, basi na pauni milioni 2 ambazo si haba, ziokolewe.
 
Hilo ni moja la kujifunza kwa klabu za hapa nyumbani namna ambavyo mikataba inaandaliwa kitaalamu na inakuwa imelenga mambo kadhaa na hata ukivunjika. Zaidi unalenda kwenye kufanikiwa na kufeli na si ilimradi mkataba tu wa kazi, hata wa kocha unaringana na wafanyakazi wote!
 
Kitu cha pili cha kujifunza ni baada ya Moyes kumalizana na Man United na kuvunja mkataba, hakuna ubishi ilikuwa ni lazima aondoke na kwenda kupumzika nje ya England.
Moyes alichagua Marekani, aliona ingekuwa sehemu nzuri ambayo angeweza kujipumzisha kabla ya kuanza upya maisha ya mapambano.
 
Kwa kuwa aliamua kwenda katika Mji wa Florida akiwa na mkewe na baada ya kulijua hilo, bilionea Glazer alimpa Moyes ofa nyingine ya kufikia katika nyumba yake ya kifahari iliyo mjini humo.
 
Pia atapata huduma ya usafiri na usimamizi wa kutembezwa sehemu mbalimbali za jiji hilo na wasaidizi wa Glazer.
Utaona hivi, kocha akivunja mkataba au klabu kufanya hivyo. Basi uadui unatangulia na ikiwezekana viongozi wa klabu hawataki hata kuzungumza na kocha kwa kuwa anaonekana kama ni adui.
 
Glazer ndiye anayepitisha uamuzi wa mwisho, lakini anaonyesha kiasi gani walivyoachana kistaarabu na Moyes na hakuna tatizo lolote lililotokea.
Hivyo mambo yako kitaalamu zaidi ndiyo maana wakati mashabiki wanaendelea kupiga kelele. Moyes anakula ‘bata’ Marekani. 
Na Saleh Ally Kutoka saleh jembe blog

0 comments: