Saturday 1 June 2013

WABUNGE WA CHADEMA NA CUF WAKUBALI KUOMBANA LADHI

Dodoma. Vyama vya CUF na Chadema vimekubali kuombana radhi ili mgogoro baina yao uishe baada ya misimamo ya pande zote kuvunja kikao cha Bunge mara mbili, juzi.
Kutokana na maridhiano hayo, Bunge leo litaendelea na mjadala wa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, baada ya kukwamishwa mara mbili na mzozo huo.
Mzozo huo ulizuka baada ya hotuba iliyoandaliwa na Chadema na kusomwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa wizara hiyo, Ezekiel Wenje kudai kuwa CUF inafuata itikadi za Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni kupigania haki za ndoa za jinsia moja yaani ‘usagaji’ na ‘ushoga’.
Vyama hivyo vyote viliombana radhi bungeni ili kumaliza mzozo huo, baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuamuru pande zote kufanya hivyo kulingana na ushauri wa Kamati ya Maadili ya Bunge.
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliomba radhi kwa upande wa Chadema, wakati upande wa CUF aliomba Mnadhimu Mkuu wa chama hicho Bungeni, Rashid ally Abdalah.
Pamoja na maombi hayo ya msamaha, pande zote ziliendelea kusimamia misimamo yao, lakini wakasema wanazingatia masilahi ya taifa kwa kuombana radhi ili Bunge liendelee kujadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Kuhusu kuihusisha CUF na sera zilizotajwa na kuleta tafrani, Mbowe alisema: “Yapo mengi ya (wabunge) kuyajadili. Hili (la ushoga na usagaji) siyo muhimu. Yapo mengi yenye masilahi kwa taifa. Bunge limeahirishwa pasipo sababu ya msingi,” alisema Mbowe na kuomba radhi.
Abdalah alikiri kuwa kauli ya Chadema ilizua mtafaruku na hasira kwa wabunge wa Chama chake na hata kujikuta wakifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu.
“Damu ilichemka na kusababisha kutoa maneno ambayo hayafai Bungeni. Naomba radhi kwa hayo,” alisema Abdalah.
Kuomba radhi huko kulitokana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Bunge, John Chiligati kueleza kuwa baada ya kuzungumza na pande zote pamoja na kufuata ushauri wa wabunge mbalimbali walibaini pande zote zina makosa.
Chiligati alisema katika mahojiano, CUF ilikiri kuwa inafuata sera za Kiliberali lakini siyo zote ikiwamo hiyo ya ushoga na usagaji, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania haikubaliani na tabia ya namna hiyo.
Kwa sababu hiyo, Chiligati alisema Chadema itaomba radhi baada ya kubainika kufanya makosa mawili wakati CUF itaomba radhi kwa vipengele vya makosa manne.

0 comments: