SIKU moja baada ya kufichua udhaifu uliopo katika
vitabu vya elimu ya msingi nchini, mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), ameitaka serikali kuwashtaki wahusika kama
wahujumu uchumi.
Pia ametaka
mamlaka husika kusimamisha mchakato wa kuvisambaza vitabu hivyo ili kutoa
nafasi ya utayarishaji wa vingine vyenye ubora unaostahili.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa
wa NCCR-Mageuzi, alisema vitabu hivyo havina ubora unaostahili na hivyo
kuruhusu visambazwe ni kuwalisha watoto sumu.
Huku akionyesha
machapisho ya vitabu tofauti, Mbatia alisema udhaifu wa vitabu hivyo unatokana
na mambo makuu matano ambayo ni sera ya elimu ya mwaka 1995 iliyotumika katika
utayarishaji wake kuwa dhaifu.
Vitabu
vimetayarishwa bila ya kutumia mitaala, mihtasari ya mwaka 2005 iliyotumika
katika utayarishaji kuwa mibovu, taratibu za kitaifa na kimataifa za
utayarishaji kutofuatwa.
Mbatia alisema
kuwa serikali ina ndimi mbili kama nyoka katika sakata hilo
na kwamba juzi Waziri Shukuru Kawambwa na naibu wake, Philipo Mulugo, walijibu
suala hilo
kisiasa ili kujiokoa bungeni.
Mbunge huyo
aliyeambatana na wabunge wenzake, David Kafulila wa Kigoma Kusini na Felix
Mkosamali wa Mhambwe, aliongeza kuwa serikali inajikanganya kwa kusema
wamebaini makosa hayo wanayoyaita madogo lakini wanakubali kuivunja EMAC.
Alisema
taratibu za utayarishaji wa vitabu ni wa hovyo kwani kuna vitabu visivyo na
mwandishi, jina la mwandishi ni kampuni ya uchapishaji.
Katika
mtiririko huo wa udhaifu wa vitabu hivyo na mihtasari, Mbatia alinukuu mitaala
ya elimu ya msingi na awali akisema ule wa msingi umeandika kuwa elimu hiyo ni
kwa ajili ya mwanafunzi kuweza kupata uelewa wa lugha ya Kifaransa
itakayomwezesha kupata ajira.
Na kwa elimu ya
awali mtaala unasema ni kumwezesha mwanafunzi kukua kiuchumi, kisiasa na
kijamii.
Alisema kuwa
kwa udhaifu huo, kamwe hawawezi kukubali fedha hiyo itumike kuangamiza taifa
kwa kusambaza vitabu hivyo ambavyo ni sawa na kuwalisha watoto sumu.
Akichangia
hotuba ya bajeti ya wizara ya elimu juzi, Mbatia alionyesha vitabu kadhaa
bungeni huku akitaja makosa mengi yaliyomo na kuhoji viliidhinishwaje na EMAC.
Mbatia alitoa
mfano wa kitabu cha Jiografia cha darasa la sita ambacho kimekosewa kwa
kuandikwa Jografia.
Vitabu vingine
ni cha hisabati cha darasa la nne katika ukarasa wa 49, ambapo kimeandikwa
sifuri gawanya kwa sifuri jibu lake
ni sifuri wakati jibu
sahihi ni haiwezekani.
Pia alisema
kitabu cha hisabati kingine kinaonyesha 2x7=15 na kitabu cha Uraia pia
kinaeleza Mtaa kuwa unaundwa na vitongoji mbalimbali na kuongozwa na wenyeviti
wa vitongoji.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment