Wednesday 12 June 2013

MWANAUME AUWAWA NA BABA YAKE MDOGO KWENYE MATANGA

 
MWANAMUME mmoja alifariki usiku wa kuamkia Jumatatu baada ya kushambuliwa na babake mdogo wakati wa matanga kwa madai ya kuhusika katika uchawi katika Kaunti ya Kilifi.
Kisa hicho kilichowaacha waombelezaji vinywa wazi kwa mshangao kilitokea katika kijiji cha Kabateni, wilayani Kaloleni.

Marehemu ambaye alitambuliwa kama Sammy Mdigo na baba wa watoto wawili yadaiwa alidungwa kisu kifuani na babake mdogo  Sharrif Charo na kufariki papo hapo baada ya malumbano ya kinyumbani kuzuka kati yao.
Mshukiwa huyo hatimaye alitoweka na hajulikani aliko hadi sasa lakini polisi wameanzisha juhudi za kumtafuta.
Duru za kuaminika zasema kwamba ugomvi ulizuka kati ya watu hao wawili huku mshambulizi akisema babake marehemu alikuwa mchawi.
Kulingana na mwanakijiji mmoja Douglas Riziki, mshukiwa alidai kuwa kakake ambaye ni marehemu alikuwa amerogwa na babake Charo hivyo basi akaamua kulipiza kisasi. 
Kisa hicho kilitokea wakati wa matanga ya marehemu kakake Charo ambayo yalikuwa yamehudhuriwa na watu wa familia na wanakijiji.
Chifu wa kata ya Mwanamwinga, Joseph Kapalia, alithibisha kisa hicho huku akisema visa vya mashambulizi kwa madai ya uchawi vimeshuhudiwa kwa muda mrefu mno eneo hilo na yafaa vikomeshemwe kwani vinarudisha maendeleo nyuma
Uchawi
“Wakaazi wengi wa hapa wanaamini sana mambo ya uchawi hali ambayo inaathiri shughuli za maendeleo na inafaa ikemewe na kukomeshwa kabisa,” akasema Kapalia.
Chifu huyo aliwasihi watu wa eneo hilo wasichukue sheria mikononi mwao na badala yake wawe na utulivu na waache polisi walishughulikie jambo hilo.  
Ndugu zake marehemu walishikwa na ghadhabu na kutaka kumshambulia mkewe mshukiwa Asha Mohammed ambaye alilazimika kutorokea kwao kwa kuhofia usalama wake.
Mwili wa marehemu ulichukuliwa na polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya St. Lukes, Kaloleni.

 Na JAMES MUCHAI Na ELINA KABIBI

0 comments: